Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katu tusikubali ufisadi ukwamishe SDGs- Guterres

Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasitoe hela kwa madaktari kwa huduma yoyote.
UNICEF/Pirozzi
Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasitoe hela kwa madaktari kwa huduma yoyote.

Katu tusikubali ufisadi ukwamishe SDGs- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kupinga rushwa na ufisadi duniani, Umoja wa Mataifa unataka hatua bunifu zaidi kushinda vita hivyo ambavyo vinapora rasilimali muhimu kwa ajili ya maendeleo  ya wananchi. Brenda Mbaitsa na maelezo zaidi.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa rushwa ni janga kwa kuwa kila mwaka matrilioni ya dola sawa na zaidi ya asilimia 5 ya pato la ndani duniani, hulipwa kama rushwa au huibwa kupitia vitendo vya kifisadi vinavyokandamizi utawala wa kisheria na kusaidia uhalifu kama vile usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya na silaha.

Amesema ukwepaji kodi, utakatishaji wa fedha na utoroshaji wa aina yoyote wa fedha hukwamisha ujenzi wa shule, hospitali na miundombinu muhimu inayohitajika kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

“Watu wana haki ya kuwa na hasira. Rushwa inatishia ustawi wa jamii zetu, mustakabali wa watoto wet una afya ya sayari yetu ya dunia. Lazima vita dhidi ya rushwa vipiganwe na wote kwa ajili ya wote,”  amesema Katibu Mkuu.

Ameenda mbali akipigia chepuo vijana akisema kuwa, kama vile wanavyohamaisha kuchukuliwa kwa hatua mujarabu kwa tabianchi na utandawazi ulio na usawa, vivyo hivyo vijana wanataka uwajibikaji na haki katika kushughulikia na kutokomeza vitendo vya rushwa.

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu Guterres anasema, “lazima tuungane dhidi ya rushwa na tukomezesha utoroshaji wa rasilimali. Mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa ulioridhiwa na takribani kila nchi duniani, unatupatia njia za kuiamarisha azma yetu ya kushughulikia tatizo hili.”

Amekumbusha kuwa baadaye mwezi huu, serikali zitakutana Abu Dhabi kutathmini maendeleo na kuandaa kikao maalum cha kwanza kabisa cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kukabili rushwa kitakachofanyika mwaka 2021.

Guterres amesihi serikali hizo zichukue uamuzi thabiti ili kupatia kipaumbele suala la kukabiliana na rushwa.

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Tijjan Muhammad-Bande amesema siku ya leo ni fursa ya kutambua na kusongesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi duniani kote.

Amekumbusha kuwa kwa mujibu wa mpango wa utekelezaji wa Addis Ababa, kuhusu  ufadhili kwa maendeleo, nchi zinatakiwa kutokomeza rushwa ili kuwepo na matumaini ya kufanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu.