Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 30 iliyopita imeshuhudia hatua katika vita dhidi ya ufisadi:UNODC

Bango lenye ujumbe wa ufisadi nchini Namibia
Bank ya Dunia/Philip Schuler
Bango lenye ujumbe wa ufisadi nchini Namibia

Miaka 30 iliyopita imeshuhudia hatua katika vita dhidi ya ufisadi:UNODC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mkutano wa kimataifa wa kujadili mkataba wa kupambana na ufisadi umeanza leo Abu Dhabi huku ikielezwa kwamba kumekuwa na hatua zilizopigwa katika vita dhidi ya changamoto hiyo ambayo sio tu ni adui wa haki bali pia adui wa maendeleo.

Umoja wa Mataifa umesema umedhamiria kupambana na ufisadi ambao ni mtihani unaozikumba nchi zote duniani kwa njia moja au nyingine, na utafanya hivyo kupitia ofisi yake ya madawa na uhalifu UNODC.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi ndio chombo pekee kinachobana kisheria dhidi ya ufisadi au rushwa na nyenzo muhimu ya kusaidia kuunda mbinu za kukabiliana na jinamizi hili kimataifa.

Asilimia kubwa ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wameridhia mkataba huo. Akizungumza na UN News kuhusu changamoto hii ya ufisadi na mkataba wa kuudhibiti, John Brandolino, mkurugenzi wa idara ya mikataba kwenye ofisi za UNODC amesema anatiwa moyo na mabadiliko ya fikra kuhusu ufisadi ukilinganisha na miaka 30 iliuopita, "sasa miaka 30 baadaye mazingira ni tofauti kabisa watu wamedhamiria kote duniani, hakuna nchi mwanachama au serikali itakayothubutu kusema ufisadi ni mzuri katika mfumo wowote ule, kila mmoja anatambua haja ya kupambana nao kwa pamoja duniani kote . Na tumepiga hatua ya jinsi ya kupambana na ufisadi tumepata njia mbalimbali ambazo tunadhani zinaweza kusaidia katika kuzuia lakini pia kwa vyombo vya sheria na ushirikiano wa kimataifa.”

Bwana Bandolino amesema licha ya hatua zilizopigwa dunia sibweteke bado kibarua kipo katika kutokomeza ufisadi, “nadhani bado kuna mengi ya kufanya kwa sababu ni suala muhimu na kwa sababu linaingiliana na mambo mengi tunayofanya na malengo yetu ya kimataifa ikiwemo malengo ya maendeleo endelevu na litaendelea kuwa katika ajenda ya juu na zaidi katika ajenda ya juu ya kimataifa.”