Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNICEF na Canada kupunguza safari za wazazi kusaka vyeti vya kuzaliwa vya watoto Haiti

 Gergens Dominique na mkewe Gedinise Edmond baada ya kumsajili mtoto wao na kupatiwa cheti cha kuzaliwa katika kituo cha usajili vizazi cha  Anse d'Hainault, nchini Haiti.
© UNICEF/Medhid Meddeb
Gergens Dominique na mkewe Gedinise Edmond baada ya kumsajili mtoto wao na kupatiwa cheti cha kuzaliwa katika kituo cha usajili vizazi cha Anse d'Hainault, nchini Haiti.

Mradi wa UNICEF na Canada kupunguza safari za wazazi kusaka vyeti vya kuzaliwa vya watoto Haiti

Haki za binadamu

Nchini Haiti, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa ufadhili kutoka Canada, wanaanzisha mradi wa kusogeza karibu na makazi ya wananchi huduma za usajili wa watoto ili wapatiwe vyeti vya kuzaliwa katika taifa hilo ambalo mtoto mmoja katiya 6  hana cheti cha kuzaliwa
 

Kwa sasa hali si hali kwa kuwa wazazi nchini Haiti wakiwemo Gergens Dominique na mkewe Gedinise Edmond wanalazimika kufunga safari nyakati za asubuhi kuelekea ofisi ya vizazi na vifo ili kusajili watoto wao na kisha wapatiwe vyeti vya kuzaliwa.
Gerdens ambaye ni mvuvi anasema, “tunapoteza muda mwingi sasa kuja huku na ni mbali, siku nzima ya kazi inapotea. Iwapo tungalikuwa na ofisi ya usajili wa watoto hospitalini, ingalikuwa bora zaidi kwangu. Iwapo ofisi wa usajili angalikuja nyumbani, ingalikuwa bora kwetu na tusingalilazimika kusafiri hadi ofisi ya usajili.”

Gedinise ni mama wa mapacha Betchie na Betchina, ambao wana umri wa miezi mitatu, kwake yeye vyeti vya kuzaliwa ni muhimu mno kwa kuwa, "kitu cha kwanza unachoulizwa ni cheti cha kuzaliwa. Nataka kuwasajili kwa kuwa watakapoenda shuleni, wataulizwa cheti cha kuzaliwa. Halikadhalika chanjo na ubatizo wanahitaij cheti cha kuzaliwa, vile vile kwa hati ya kusafiria cheti cha kuzaliwa ni muhimu. »
Nats.
Msajili akatangaza cheti cha Betchina kiko tayari. Msajili huyu Jean-Félix Dumas, ndiye pekee kwa ajili ya wakazi 37,000 wa mji wa Anse d’Hainault naye anasema, « nimeanza kuzeeka, macho yangu hayaoni vizuri. Ni afisa usajili pekee kwa mji wote wa Anse d’Hainault na sitoshelezi. Inatakiwa maafisa wengine.Mfano nikiugua, ofisi inafungwa. »

Canada imesikia kilio na hivyo kuunga mkono mradi wa UNICEF wenye lengo la kusajili watoto 298,000 kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2022.

Claude Mane Das, Mtaalamu wa masuala ya ulinzi wa mtoto, UNICEF nchini Haiti anasema, « lengo la mradi ni kwenda mbali zaidi. Inapaswa kufikia asilimia 100 ya usajili wa vizazi. Inahitajika ofisi ya usajili wa vizazi ndani ya hospitali. Halikadhalika kwenda maeneo ya ndani zaidi. Maafisa usajili na makarani wanapaswa kuwa karibu zaidi na watu ili watoto wote waweze kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Tunatumaini kwamba hadi mwaka 2025 tutakuwa tumesajili watoto wote Haiti na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa. »

Ibara ya 7 kipengele cha kwanza cha mkataba wa kimataifa wa  haki za mtoto, CRC, unaeleza bayana kuwa “mtoto anapaswa kusajiliwa punde tu baada ya kuzaliwa na atakuwa na haki ya kupatiwa jina, haki ya kupatiwa utaifa na kadri iwezekanavyo haki ya kutambua na kulelewa na wazazi wake.”