Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usajili wa kuzaliwa ni nini na una umuhimu gani?

Mtoto wa umri wa miezi mbili apokea cheti cha kuzaliwa mjini Accra,Ghana.
UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto wa umri wa miezi mbili apokea cheti cha kuzaliwa mjini Accra,Ghana.

Usajili wa kuzaliwa ni nini na una umuhimu gani?

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katika nchi nyingine, usajili wa kuzaliwa haupewi kipaumbele kama jambo la kawaida kufuatia kuzaliwa kwa mtoto. Lakini kwa wengine wengi, ni hatua muhimu inayokosekana katika kuthibitisha utambulisho wa kisheria wa mtoto. Bila huo, watoto hawatambuliki na serikali zao, hivyo haki zao zinaweza kutolindwa na kutozingatiwa, pamoja na huduma muhimu kama huduma za afya na elimu.

Karibu robo ya watoto wote waliozaliwa duniani walio chini ya wa miaka 5 hawajawahi kusajiliwa. Maisha ya watoto hawa ni muhimu, lakini hawawezi kulindwa ikiwa serikali hawatambui.

Usajili wa kuzaliwa ni nini?

Mtoto wa umri wa miezi mbili apokea cheti cha kuzaliwa mjini Accra,Ghana.
UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto wa umri wa miezi mbili apokea cheti cha kuzaliwa mjini Accra,Ghana.

 

Usajili wa kuzaliwa ni mchakato wa kuandikisha kuzaliwa kwa mtoto. Ni rekodi rasmi na ya kudumu ya kuwepo kwa mtoto, na hutoa utambulisho wa kisheria wa mtoto huyo.

Kwa kiwango cha chini, huweka rekodi ya kisheria ya mtoto alikozaliwa, utambulisho wa wazazi wake. Usajili wa kuzaliwa unahitajika ili mtoto apate cheti cha kuzaliwa , ni dhibitisho lake la kwanza la kisheria la utambulisho.

Usajili wa kuzaliwa si tu haki ya msingi ya binadamu, bali pia husaidia kuhakikisha kuwa haki zingine za watoto zinazingatiwa, kama vile haki za kulindwa dhidi ya dhuluma, na kupata huduma muhimu za kijamii kama utunzaji wa afya na haki. Habari zinayokusanywa kutoka kwenye takwimu za usajili wa kuzaliwa husaidia serikali kuamua wapi na jinsi ya kutumia pesa, na maeneo gani ya kuzingatia katika programu za maendeleo, kama vile elimu na chanjo.

Kuna tofauti gani kati ya usajili wa kuzaliwa na cheti cha kuzaliwa?

Kwa kina, usajili wa kuzaliwa ni mchakato wa kutambulisha rasmi kuzaliwa na mamlaka ya serikali, na cheti cha kuzaliwa ni karatasi iliyotolewa na serikali kwa mzazi au mlezi kwa ajili ya mchakato huu. Cheti cha kuzaliwa kinathibitisha kuwa usajili umefanyika.

Usajili wa kuzaliwa na cheti cha kuzaliwa kweli vinaenda sambamba. Walakini, kwa sababu michakato ya utoaji wa cheti cha kuzaliwa inaweza kutofautiana kulingana na eneo, mtoto anaweza kusajiliwa lakini kamwe asipate cheti cha kuzaliwa

 

Tegene Erke anamsajili binti yake wa miezi tisa Alemtsehay Chele. Wanaishi katika mkoa wa Amhara wa Ethiopia, ambao ulianzisha Wakala wa Usajili wa muhimu mnamo mwaka 2016. Katika mwaka wake wa kwanza, ilisajili asilimia 78 ya Watoto ambayo ni rekodi muhimu. Tangu wakati huo, mkoa huo ukawa kielelezo cha kuigwa kwa mikoa mingine nchini Ethiopia.

 

 

 

Ni nini hufanyika ikiwa mtoto hajasajiliwa?

Usajili wa kuzaliwa ndiyo njia pekee ya kisheria kwa mtoto kupata cheti cha kuzaliwa.

Uthibitisho huu wa kisheria wa utambulisho unaweza kusaidia kulinda watoto dhidi ya dhuluma na unyanyasaji. Bila cheti cha kuzaliwa, watoto hawawezi kudhibitisha umri wao, na hivyo inawaweka katika hatari kubwa zaidi ya kulazimishwa kuingia kwenye ndoa za mapema au soko la ajira, au kusajiliwa katika vikosi vya jeshi.

watoto wakisajiliwa inaweza pia kusaidia kuwalinda watoto wahamiaji na wakimbizi dhidi ya kutengwa na familia, na usafirishaji haramu. Bila usajili huo, watoto hawa wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kutokuwa na uraia, hivyo  hawana uhusiano wa kisheria na nchi yoyote, pamoja na utaifa.

Bila cheti cha kuzaliwa, watoto wengi hawawezi kupata chanjo, taratibu na huduma zingine za afya. Wanaweza kukosa kuhudhuria shule au kujiandikisha kwenye mitihani. Hii inasababisha fursa zao za kazi za baadaye kupungua na kuwafanya waishi katika umaskini.

Katika utu uzima, watoto watahitaji kitambulisho hiki rasmi kwa shughuli za msingi na muhimu kama kufungua akaunti za benki, kujiandikisha kupiga kura, kupata pasipoti, kuingia katika soko rasmi la kazi, kununua au kurithi mali, au kupokea msaada wa kijamii.

Ni watoto wangapi hawajasajiliwa?

Usajili wa kuzaliwa umeenea kote katika nchi nyingi tajiri. Lakini katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, kwa wastani, mtoto mmoja kati ya wanne wa chini ya miaka 5 ( sawa na watoto milioni 166 hawajasajiliwa. Kati ya watoto hao milioni 166, nusu wanaishi katika nchi tano tu: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Ethiopia, India, Nigeria na Pakistani.

Hata wakati ambapo watoto wamesajiliwa, wanaweza kukosa udhibitisho wa usajili. Takriban watoto milioni 237 wa chini ya umri wa miaka 5 ulimwenguni kote sasa hawana cheti cha kuzaliwa.

Nchini Myanmar, watoto wenye umri wa hadi miaka kumi wanaweza sasa kusajiliwa mjini kwa bila hitaji la kumwona mkuu wa afya nchini
UNICEF/Nyan Zay Htet
Nchini Myanmar, watoto wenye umri wa hadi miaka kumi wanaweza sasa kusajiliwa mjini kwa bila hitaji la kumwona mkuu wa afya nchini

 

“Watoto wangu wote tayari wana vyeti vyao vya kuzaliwa. Anasema mama huyu kutoka Myanmar Hapo awali haikuwa rahisi kama haujasajili watoto wako kabla ya kutimiza umri wa mwaka moja. Sasa, walisema hadi watoto watakapofikisha miaka 10, wataweza kusajiliwa katika vitongoji vyao bila haja ya kwenda kwa mkurugenzi wa afya wa serikali,”

Je! Kwanini sio watoto wote ambao wanasajiliwa wakati wa kuzaliwa?

Kuna sababu nyingi kwa nini watoto hawasajiliwi. Katika mazingira mengi watoto hawa wanaishi katika kaya masikini, mara nyingi katika maeneo ya vijijini kwenye upatikanaji mdogo wa huduma za usajili, au katika nchi zaidi ya 100 zisizo na mifumo kamili ya usajili wa raia.

Katika hali zingine, wazazi wanaweza kuwa hawatambui usajili wa kuzaliwa au wanaweza kutoelewa umuhimu wake. Gharama pia ni kizuizi muhimu kwani wazazi wanaweza kukosa kumudu gharama zinazohusiana na usajili, pamoja na kusafiri kwenda kwenye maeneo ya usajili au faini ya kuchelewa kusajili.

Baadhi ya vikundi vya watu vya kikabila au kidini vina viwango vya chini vya usajili kuliko wastani wa kitaifa. Hii inaweza kuwa ni kwa sababu tamaduni zao huweka msisitizo zaidi kwa mila zingine kama sherehe za kuwapa watoto majina,  au kwa sababu vikundi hivi vya watu vimetengwa, mara nyingi huishi katika maeneo ya mbali au hawajatambuliwa na serikali zao.

Na katika nchi kadhaa, wanawake hawana haki sawa na wanaume linapokuja suala la kusajili watoto wao. Wengine hawawezi kusajili watoto wao wakati wowote, wakati wengine wanaweza tu kufanya hivyo na baba mzazi akiwepo.

Ni jinsi gani usajili wa kuzaliwa ni suala la usawa wa kijinsia?

Katika sehemu nyingi za ulimwengu, wanawake hawana haki sawa au uwezo wa kusajili kuzaliwa kwa mtoto kama wanaume. Bado kuna nchi 25 ambapo wanawake hawana haki sawa na wanaume kupitisha kisheria utaifa wao kwa watoto wao. Aina hii ya ubaguzi wa kijinsia katika sheria na sera za kitaifa zinahitaji kupitiwa na kurekebishwa ili kuondoa athari mbaya kwa jamii.

Mama anaweza kukabiliwa na ubaguzi wa kijinsia anapojaribu kusajili mtoto wake, kwa sababu kama vile kutokuwa na kitambulisho au cheti cha ndoa, au ikiwa baba mzazi hakuwepo au kutajwa katika fomu ya kuzaliwa.

Wanawake wanaweza kukosa kusajili watoto wao ikiwa baba hajulikani, au ikiwa anakataa kutambua ukoo kama vile katika visa vya waathirika wa ubakaji au uchumba.

Kutosajiliwa wakati wa kuzaliwa pia kunaweza kuongeza mapengo ya kijinsia yaliyopo katika maeneo kama elimu. Ulimwenguni kote, wasichana milioni 132 wameacha shule, na wasichana hawa wana uwezekano mkubwa wa kutorejea shuleni kuliko wavulana walioacha shuleni. Kutokuwa na cheti cha kuzaliwa hufanya iwe ngumu zaidi kwao kuenda shuleni. Na wasichana wasio na vyeti vya kuzaliwa ambao hawawezi kudhibitisha umri wao pia wako katika hatari zaidi kujikuta katika ndoa za utotoni, na hivyo kutotimiza masomo yao.

 

Mtoto mchanga anatambuliwa kabla ya usajili wa kuzaliwa katika Hospitali Kuu ya San Juan de Dios katika mji la Guatemala, Guatemala.

Viwango vya usajili wa kuzaliwa vinawezaje kuboreshwa?

Utambulisho wa kisheria, pamoja na usajili wa kuzaliwa, ni haki ya binadamu. Ili kila mtoto kutekeleza haki hii, serikali lazima ziboreshe na kuimarisha mifumo ya usajili wa raia.

Kuboresha viwango vya usajili wa kuzaliwa kunaweza kufanywa kwa njia kadhaa, pamoja na kuondoa ada ya usajili na faini ya kuchelewa, au kutoa ruzuku ya pesa kwa familia zinaowaandikisha watoto wao. Kuongeza idadi ya wasajili, na/au kuwatuma katika maeneo ya mbali katika vitengo vya usajili pia kunaweza kusaidia serikali kufikia idadi kubwa ya watu walioko hatarini.

Teknolojia ni pendekezo lingine la suluhisho. Serikali za Pakistani na Tanzania zimezindua programu za simu za usajili wa kuzaliwa, ambazo zinaruhusu wasajili kukusanya takwimu kwa njia ya digitali na kupakia takwimu hizo za usajili kwenye mfumo wa serikali kwa wakati halisi.

Mwishowe, tunahitaji kufanya usajili wa kuzaliwa kuwa zoezi la kawaida katika jamii ambazo haufanyiki kila wakati. Hii inamaanisha kushawishi serikali kurekebisha sheria na sera zao, na kufanya kazi na jamii kubadili mitazamo na tabia hivyo kuonyesha thamani na faida za usajili wa kuzaliwa ili kukidhi mahitaji yake.

 

 

Je, UNICEF inafanya nini kusaidia?

UNICEF imekuwa msitari wa mbele katika usajili wa kuzaliwa ulimwenguni kwa zaidi ya miaka 30. Mnamo mwaka 2018, tulifanya kazi na serikali na jamii na kusajili watoto waliozaliwa zaidi ya milioni 16 na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watu zaidi ya milioni 13.

Kazi yetu inazingatia kusaidia serikali kuimarisha mifumo yake ya usajili wa raia. Hii ni pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya huduma ambapo watoto wanaweza kusajiliwa, kukuza au kuunda sera za usajili wa kuzaliwa, uvumbuzi katika teknolojia ya usajili, na kuzidisha uhamasishaji wa jamii kihusu usajili wakati wa kuzaliwa.

Pia tunafanya kazi na sekta zingine, kama afya na elimu, kuunganisha usajili wa kuzaliwa katika kazi zao. Hii ni pamoja na kuzidisha usajili wa kuzaliwa katika hospitali na vituo vya afya, pamoja na usajili wa kuzaliwa kwenye mazoezi ya chanjo, na kuunganisha mifumo ya usajili wa kuzaliwa na mfumo wa kitaifa wa kuhamisha pesa na kuhifadhi takwimu za wanafunzi.

Ulimwengu umepiga hatua kubwa kwenye usajili wa kuzaliwa kwa miaka 20 iliyopita. Hivi leo, karibu asilimia 75 ya watoto wa chini ya umri wa miaka 5 wamesajiliwa, ikilinganishwa na asilimia 60 mwaka 2000. Bila maendeleo haya, watoto milioni 100 hawangesajiliwa leo hii.

Lakini nchi zinahitaji uwekezaji zaidi na kujitolea kufanikisha usajili wa kuzaliwa kwa wote ifikapo 2030.