Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila cheti cha kuzaliwa nisingefika London-Shopna

Watoto wakimbizi kutoka Mali waliozaliwa kambi ya Mbera nchini Mauritania wakipatiwa hati ya cheti cha kuzaliwa.
UNHCR
Watoto wakimbizi kutoka Mali waliozaliwa kambi ya Mbera nchini Mauritania wakipatiwa hati ya cheti cha kuzaliwa.

Bila cheti cha kuzaliwa nisingefika London-Shopna

Haki za binadamu

Benki ya dunia inasema takribani watu bilioni moja kote duniani, hawana utambulisho rasmi, jambo ambalo linawapa ugumu kupata huduma muhimu kama vile afya, elimu na huduma za kifedha.

Shopna akiwa na umri wa miaka 12 alikikimbia Kijiji chake na kuingia katika mitaa ya mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka baada ya wazazi wake kumlazimisha kuolewa. Ilikuwa aikose fursa ya kwenda London kushiriki katika mchezo aupendao wa kriketi kama siyo mradi wa mpango wa utambuzi, ID4D unaodhaminiwa na Benki ya Dunia kupitia mashirika mbalimbali.

Fainali za michuano ya kwanza ya kombe la dunia la kriketi inayowahusisha watoto wanaotoka katika mazingira magumu inakamilika hii leo mjini London Uingereza.

Kombe la dunia la kriketi linawaleta pamoja watoto kutoka kote duniani katika timu 10 za wasichana na wavulana ili waziwakilishe nchi zao na baada ya michuano kupaza sauti na kutoa maoni ya kusaidia kuboresha maisha ya watoto wa mitaani kote duniani.

Lakini watoto wengi zaidi wanashindwa kushiriki fursa kama hizi kutokana na kukosa vyeti vya kuzaliwa na hivyo kukosa utambulisho wa utaifa ambao hatimaye ungewapatia hati za kusafiria.

Kutokana na msaada wa benki ya dunia, Shopna ameweza kupata cheti cha kuzaliwa ambacho kinamkinga na ndoa za utotoni na pia ameweza kupata hati ya kusafiria ambayo imempa nafasi ya kusafiri hadi London kushiriki michuano ya kombe la dunia la Kriketi kwa watoto waishio mitaani.

“Nilikipenda Kijiji changu lakini nililazimika kuondoka na kuja kuishi katika kituo cha treni ambako ni hatari kwa wasichana. Shirika la Leedo waliniokoa, wakanipa makazi salama wakanisaidia kupata cheti cha kuzaliwa.” Anasema Shopna.

Kisha anaongeza,“lengo langu ni kuwa daktari ndiyo maana nilikataa kuolewa. Cheti changu cha kuzaliwa kuzaliwa kinathibitisha umri wangu, kinanilinda dhidi ya ndoa za utotoni. Ninayo furaha lkushiriki katika michuapo hii.”

Miongoni mwa watoto wanaoshiriki michuano hiyo ya utangulizi kabla ya michuano ya kimataifa ya ubingwa wa Kriketi yaani ICC Cricket World Cup, wanatoka katika nchi za Napol, Bangladesh, DRC na Tanzania.