Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 166 hawatambuliki kwa kutosajiliwa baada ya kuzaliwa:UNICEF

Serikali ya Kenya ilipotoa  vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 600 kutoka jamii ya Washona, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwalinda na hatua ya kwanza kuelekea kumaliza tatizo la utaifa kwa watu 3,500 nchini humo.
UNHCR/Rose Ogola
Serikali ya Kenya ilipotoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 600 kutoka jamii ya Washona, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwalinda na hatua ya kwanza kuelekea kumaliza tatizo la utaifa kwa watu 3,500 nchini humo.

Watoto milioni 166 hawatambuliki kwa kutosajiliwa baada ya kuzaliwa:UNICEF

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, inasema kushindwa kuwasajili watoto wachanga pindi wanapozaliwa kumesababisha kuwaacha mamilioni ya watoto bila kutambulika.

Ripoti hiyo inasema ingawa idadi ya watoto waliosajiliwa pindi baada ya kuzaliwa imeongezeka kwa kiasi kikubwa, bado kuna watoto milioni 166 wa umri wa chini ya miaka 5 hawajasajiliwa huku wengine milioni 237 hawana vyeti vya kuzaliwa na hivyo kuwaacha katika hali tete ya kutotambulika.

Ripoti hiyo mpya ambayo inatahimini takiwmu kutoka nchi 174 inaonyesha kwamba kiwango cha watoto kusajiliwa kimataifa kimeongezeka kwa karibu asilimia 20 ikilinganishwa na muongo mmoja uliopita, lakini mtoto 1 kati ya 4 hajulikani na ana uwezekano mkubwa wa kukosa elimu, huduma za afya na huduma zingine za msingi zinazohitaji nyaraka za utambulisho.

UNICEF inasema hatua kubwa zilizopigwa kimataifa zimetokana na mafanikio yaliyopatikna Kusini mwa Asia, huku nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiburuta mkia duniani kwa kutosajili watoto wengi.

Changamoto kubwa za tatizo hilo UNICEF inasema ni matatizo yanayolikabili bara la Afrika yakiwemo ya kiuchumi , migogoro na mifumo ya huduma za jamii kama afya. Shirika hilo limesisitiza kuwa bila kuwa na nyaraka za utambulisho mbali ya kukosa huduma za msingi watoto wako katika hatari kubwa ya kutokuwa na utaifa.