Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Huduma za kibinadamu na haki za binadamu zazidi kutwama

Huduma za kibinadamu na haki za binadamu zazidi kutwama nchini Haiti..
© UNICEF/Ndiaga Seck
Huduma za kibinadamu na haki za binadamu zazidi kutwama nchini Haiti..

Haiti: Huduma za kibinadamu na haki za binadamu zazidi kutwama

Haki za binadamu

Kutoroka gerezani kwa zaidi ya wafungwa 4,500 nchini Haiti mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwemo viongozi mashuhuri wa magenge ya uhalifu kukitajwa kuwa tishio la usalama wa taifa, huku huduma muhimu kama afya, elimu zikiendelea kuzorota kila uchao, Umoja wa Mataifa unataka hatua za haraka za jamii ya kimataifa kuzuia taifa hilo kuzidi kutumbukia kwenye ghasia.

Kauli ya karibuni zaidi ni kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk ambaye hii leo amesema matumaini ya kurejesha Haiti katika hali ya kawaida yanazidi kuyeyuka kwa kuzingatia pia waliotoroka ni pamoja na watuhumiwa wa mauaji ya Rais Jovenel Moïse

Ilielezwa kuwa kutoroka kwa wafungwa hao kulitokana na  hatua za uratibu zilizopangwa na magenge ya uhalifu dhidi  ya taasisi za kitaifa kwa lengo la kuporomosha serikali. 

“Hali hii si sahihi kwa wananchi wa Haiti,” amesema Bwana Türk, akiongeza kuwa “tangu mwanzoni mwa mwaka huu watu 1,193 wameuawa na wengine 692 wamejeruhiwa kwenye ghasia zinazoendeshwa na magenge  yaliyojihami. 

Magenge yanatumikisha watoto Haiti 

Hali ya kibinadamu nayo inazorota kwani Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Haiti, Ulrika Richardson, amesema tangu tarehe 29 mwezi uliopita wa Februari, ghasia zinazosababishwa na magenge ya uhalifu zimefurusha maelfu ya raia kutoka makwao huku huduma za msingi za kijamii zikiwa haziwezi kufikiwa. 

“Zaidi ya watu 15,000 waliokuwa tayari wamefurushwa makwao, wamelazimika tena kukimbia kutokana na ghasia za hivi karibuni,” amesema Bi. Richardson akiongeza kuwa wengi wao sasa wanaishi kwenye maeneo yaliyokuweko ya hifadhi na wengine kwenye makazi yaliyoanzishwa sasa. 

Amesema ghasia za sasa lazima zikome. Mashirika ya kiutu yana hofu juu ya madhara ya ghasia zas asa kwenye hospitali, vituo vya afya na shule kwenye mji mkuu Port-au-Prince. 

Kwa sasa ni kituo kimoja tu cha afya kinafanya kazi Port-au-Prince, mamia ya shule zimefungwa au zinafanya kazi chini ya uwezo wake. 

Kwenye maeneo ambako misaada inahitaji, watoa misaada hawawezi kufika, “zaidi ya mahitaji ya kiutu, Haiti inahitaji mshikamano wa kimataifa wakati huu muhimu,” amesema Bi. Richardson. 

Kikosi cha usaidizi kipelekwe haraka

Kwa Bwana Türk,  hofu pia ni watoto kuendelea kutumiwa na magenge  ya uhalifu, shughuli za kiuchumi zikidorora kwani magenge hayo yanaweka vizuizi njiani. 

“Kwa mara nyingine tena, narejelea wito wangu wa kupelekwa haraka kwa jeshi la usaidizi kwa Haiti, kusaidia polisi wa kitaifa kurejesha usalama kwa wananchi, na kikosi hicho kiendeshe shughuli zake kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu,” amesema Türk. 

Baadaye leo, Baraza la Usalama la UN litakutana kuhusu Haiti wakati huu ambapo jamii ya kimataifa inasubiri utekelezaji wa kupeleka kikosi kitakachoongozwa na Kenya kwenye Haiti, kufuatia ombi la serikali ambalo liliridhiwa na Baraza hilo.