Ni wakati wanawake Sudan Kusini tusikilizwe japo mara moja:Mkimbizi Buchai

2 Oktoba 2020

Wanawake wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Malakal nchini Sudan Kusini wanasema wamechoshwa na vita na kupoteza watoto wao kila uchao, sasa wanaitaka serikali kupanda mbegu ya amani na kusikiliza vilio vyao japo mara moja.

Malakal kwenye makazi ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi wa raia tunakutana na Rebecca Buchai, kiongozi wa wanawake wakimbizi wa ndani katika eneo hilo lililopo jimbo la Upper Nile.

Anasema tunadai amani lakini hakuna amani, hakuna utulivu, hakuna usalama, nchi iko katika hali tete.  

Na kilio hicho si chake peke yake ni cha maelfu ya wanawake anaowawakilisha, anaamini kwamba sasa umewadia wakati kwa watu wa taifa hilo na viongozi wao kuleta amani ya kudumu kwa pamoja na kuhakikisha amani hiyo ni jumuishi ikishirikisha wote wanaume na wanawake. 

Kama mkimbizi wa ndani anatambua kwamba waathirika wakubwa kwenye machafuko yanayoendelea Sudan Kusini ni wanawake na watoto na vilio vyao huwa vinapuuzwa, sasa kwa niaba ya wanawake wenzake anataka serikali japo mara moja iwasilikilize wanawake wa sudan Kusini na kutilia maanani mahitaji yao kwa kufanya kila liwezekanalo kuleta amani na kufuta machozi yao, “tunasaka amani, tunatoa wito wa amani, na tunaitaka amani ya kweli mioyoni mwetu. Serikali lazima itujali sote na kusikiliza kilio cha wanawake japo mara moja. Watoto wetu wameachwa yatima sababu ya vita, hivyo tunataka amani nchi imesambaratika.” 

Pia Rebecca amesisitiza umuhimu wa maendeleo katika taifa hilo changa zaidi duniani kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo,“ili kuwa na mustakbali bora lazima kuwe na maendeleo, na lazima kuwe na maendeleo kwa sababu nchi yetu ina rasilimali za asili za kutosha. Endapo tutaliweka taifa letu mioyoni mwetu na kuungana tutaona. Mito ina mali asili, misitu ina maliasili , ardhi ina maliasili hususan Upper Nile, endapo tutaungana hakuna kitakachotushinda Upper Nile, tuna ardhi kubwa iliyo na kazi kwa wanaume. Wanaume hawafikirii mapigano, wanafikiria maendeleo kwa ajili ya vizazi vijavyo.” 

Kama walivyo maelfu ya wanawake Sudan Kusini ndoto ya Rebecca ni kupata amani ya kudumu Sudan Kusini na kurejea nyumbani kuunganisha familia yake iliyosambaratishwa na vita. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter