Vitendo vya kujiua Sudan Kusini vyashamiri, UNHCR yaibuka na operesheni matumaini

12 Oktoba 2018

Sudan Kusini inashuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaojiua au wanaojaribu kujiua kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takribani miaka mitano sasa, ambayo pia vimesababisha watu milioni 2 kukimbilia nchi jirani na wengine milioni 1.9 kusalia wakimbizi wa ndani nchini humo. Flora Nducha na ripoti kamili.

Huyu ni James Jafar mkazi wa jimbo la Malakal na manusura wa jaribio la kujiua. Huko Malakal alilazimika kukimbia na kuja kuishi kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani,na  aliyoshuhudia Malakal bado ni kumbukumbu akisema kuwa "Walikuwa wanaiba simu, kompyuta mpakato na fedha. Walibaka wanawake mbele ya mama na baba zao. Na ndio maana niliamua kukimbia mji huo.”

Hata maisha ya kambini kwake yeyé na mkewe na mwanae yalijaa msongo wa mawazo na akaona bora anywe pombe kupindukia,  hali iliyosababisha ugomvi wa mara kwa mara na mkewe na kwamba “ni vigumu kuhimili maisha ya kambini. Nilipofika  hapa nilikuwa mpweke. Nilibaini kuwa unywaji pombe hautatatua matatizo yangu. Niliamua kujiua. Rafiki yangu ndiye alivunja mlango na kuniokoa.”

Hali ngumu ya kambini inathibitishwa na Afisa wa wakimbizi wa UNHCR kambini hapa Alfred Lolubah akisema “hawawezi kutembea kwa uhuru kama ilivyokuwa kabla ya vita. Wamesalia tu hapa. Wanaona maisha yamefikia ukomo katika hali hii waliyojikuta nayo.”

Ili kusaidia wakimbizi kuepusha watu kujiua na kusaidia manusura wa kujiua, UNHCR imeanzisha Operesheni Matumaini. Tayari James anajitolea katika operesheni kusaidia kuliemisha vijana wasitumbukie kwenye mtego ambao yeye aliweza kuepuka.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter