Chonde chonde tufufue ahadi ya pamoja ya ushirikiano wa kimataifa:Bozkir 

22 Septemba 2020

Janga la corona au COVID-19 limewazuia viongozi wengi wa dunia kutokuja New York kuhutubia kwa uso uso mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulioanza leo, lakini Rais wa Baraza Kuu amesisitiza kwamba haja ya kufanyika mjadala huo na kukutana hata kwa mtandao ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote. 

Baada ya kufungua rasmi mjadala huo Violkan Bozkir ametoa taswira halisi ya uchumi, kuzidiwa kwa mifumo ya afya na kuingiliwa kwa mfumo wa elimu kutokana na janga la corona au COVID-19 akisema, “wale walio hatarini ndio walioathirika zaidi” ameainisha hali inayowakabili wakimbizi na wahamiaji, hatari za ukatili wa kijinsia , watoto wanaokabiliwa na unyanyasaji na kuongezeka kwa machafuko ya kikabila na kidini. 

Bozkir amesema, “ni nadra binadamu wote wanakabiliwa na tishio hilo la Pamoja, ni lazima tuweke kando tofauti zetu na kutokubaliana kwetu , tufufue ahadi yetu ya pamoja katika ushirikiano wa kimataifa.” 

Amesisitiza kwamba juhudi za Pamoja zinahitajika kutatua changamoto za kimataifa akisema sisi watu wa Umoja wa Mataifa tunaweza kulitimiza hili. 

Uhalali wa UN 

Baada ya vita vya pili vya dunia Umoja wa Mataifa ulianzishwa kama jukumu la Pamoja la kusoingesha mbele ubinadfamu amesema Bozkir na kama kitovu cha uhalali wake, ambao ni kuhakikisha amani, mafanikio na maendeleo kwa wote. 

Rais huyo wa Baraza Kuu ameongeza kuwa mfumo uliandaliwa ili kuruhusu mbadailiko “ili tuweze kushughulikia changamoto zinazojitokeza na masuala yasiyotarajiwa ikiwemo janga la sasa la COVID-19. Tunaweza kupanga, kutekeleza na kujijenga vyema kwa ajili ya kujikwamua ambako ni endelevu, jumuishi na kwa usawa.” 

Kujikwamua na janga la COVID-19 

Wakati janga la COVID-19 litaendcelea kuathiri jinsi Umoja wa Mataifa unavyofanyakazi Bwana. Bozkir amehimiza haja ya kutumia kikamilifu nyenzo zilizopo ili kupambana na changamoto hiyo ikiwemo Baraza Kuu ambalo ameliita “jukwaa muhimu la kutoa muongozo wa kisiasa.” 

Amewageukia nchi wanachama akisema “Nawatolea wito nchi wanachama kutoa ushirikiano, kuwa wabunifu na kusaka suluhu ambazo zitawezesha chombo hiki kufanya kazi yake ipasavyo na kusailia kuwa muhimu.” 

Kuongezeka kwa mahitaji 

Tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa miaka 75 iliyopita mahitaji yake yameongezeka kwa kiasi kikubwa. 

Rais wa Baraza Kuu amefafanua kwamba unaunga mkono masuala ya amani na usalama kwa kuwa na walinda amani 95,000 katika operesheni 13 za kimataifa kwenye maeneo yote yenye migogoro , inaratibu ukusanyaji wa mabilioni yad ola katika maombi ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya mamilioni ya watu wanaohitaji msaada , inasambaza chanjo kwa nusu ya Watoto wa dunia nzima, inaokoa Maisha ya watu milioni 3 kila mwaka na kuimarisha na kuchagiza ulinzi wa watu kote duniani kupitia Baraza la Haki za Binadamu. 

Na kuzuka kwa janga la COVID-19 kilichofanyika ni kuongeza shinikizo kwenye mfumo wa umoja wa Mataifa. 

UN ni muhimu kwa madhumuni yake 

Bwana. Bozkir amedai kwamba Umoja wa Mataifa unahitaji kubotresha uratibu , mshikamano, ufanisi na uwezo wa kutimiza matakwa kwa kuhusisha zaidi nguzo tatu za Umoja wa Mataifa za amani na usalama, haki za binadamu na maendeleo. 

Mshirika ya Umoja wa Mataifa ni lazima yaimarishwe amesema na “lazima tujiandae kuwa na mazungumzo magumu, ya kweli kuhusu wapi mshikamano wa kimataifa unapoingia dosari au wapi ambako wanashindwa kufuatilia haraka changamoto ambazo kwa sasa zinabadilika kila uchao kuliko wakati mwingine wowote. 

Kutoa kipaumbele kwa watu 

Bozkir amewataka wajumbe wa Baraza Kuu kufikiria watu wanaowahuhudmia kama watu binafsi na wana mahitaji tofauti kama vile mtoto ambaye elimu yake imevurugwa na janga la COVID-19 au ni muathirika wa ugaidi ambaye anahitaji msaada wa kimwili au kisaikolojia , watu hawa wanahitaji msaada wetu. 

“Mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ni mfumo mzuri uliopo kuweza kutoa suluhu kwa masuala magumu kama vile mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama, matarajio ya haki za binadamu na majanga ya kimataifa. 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud