UNWTO na UNDP wamesadia kuimarisha utalii Tanzania- TTB

21 Septemba 2020

Nchini Tanzania miaka 75 ya Umoja wa Mataifa imekuwa na manufaa kwa taifa hilo la Afrika Mashariki kupitia miradi mbalimbali ambayo chombo hicho kimekuwa kikitekeleza kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za nchi hiyo.
 

Miongoni mwa taasisi nufaika ni Bodi ya Utalii Tanzania, TTB ambayo Mkurugenzi Mwendeshaji wake Devotha Mdachi amesema wamenufaika kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la utalii, UNWTO na lile la mpango wa maendeleo, UNDP.

Bi. Mdachi amesema, “tumeweza kunufaika na mashirika hayo mawili kwa kupata miradi mbalimbali ambayo imetuwezesha kutangaza utalii wa Tanzania. Chini ya UNWTO tumeweza kuanzisha mradi ambao unasaidia katika kuendeleza utalii wa kiutamaduni, ambao kwa sasa tumeweza kusaidia jamii mbalimbali zilizo kwenye maeneo mbalimbali kuanzisha vikundi vidogo vidogo vinavyotangaza utalii wa ndani na utalii wa kitamaduni ambao kwa lugha ya kiingereza unajulikana kama Cultural Tourism Programme.”

Kuhusu miradi kutoka UNDP, Mkurugenzi Mwendeshaji huyo wa TTB amesema, “tulipata msaada ambao ulisaidia kuboresha tovuti ya bodi ya utalii. Kwa hiyo  tunatoa shukrani tukiamini kuwa uhusiano huo utaendelea kudumu miaka na miaka.”
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter