Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni miaka 75 tangu mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la UN ulipofanyika kwa mara ya kwanza. Guterres atathimini

Muonekano wa wajumbe waliokutana katika mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipofunguliwa tarehe 10 Januari 1946 katika Central Hall, Uingereza.
UN Photo/Marcel Bolomey
Muonekano wa wajumbe waliokutana katika mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipofunguliwa tarehe 10 Januari 1946 katika Central Hall, Uingereza.

Ni miaka 75 tangu mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la UN ulipofanyika kwa mara ya kwanza. Guterres atathimini

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehutubia mkutano wa kuadhimisha miaka 75 tangu mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulipofanyika mjini London Uingereza.  

Akihutubia kwa njia ya video Katibu Mkuu Guterres pamoja na kuanza kwa kuwaambia wafuatiliaji wote wa maadhimisho hayo kuwa ni heshima ya kipekee kwake kuhutubia leo katika kumbukumu ya miaka 75 ya mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika miaka hiyo 75 iliyopita, ametoa heshima kwa mmoja wa watu walioshiriki kuandaa mkutano huo, Sir Brian Urquhart ambaye amefariki dunia wiki iliyopita.  

“Mchanganyiko wa kujitolea, uadilifu na ujuzi wa kidiplomasia wa Sir Brian, viliweka kiwango kwa Umoja wa Mataifa. Ameacha alama ya kudumu katika maeneo mengi ya kazi yetu hususani kuanzishwa kwa ulinzi wa amani ambao umeokoa maisha yasiyohesabika na kupunguza mateso ya wanadamu kote duniani.” Ameeleza Bwana Guterres.  

Bwana Guterres pia amekumbushia historia ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945 mara tu baada ya vita ya pili ya dunia na hivyo msingi wake unatokana na nyakati za giza za mgogoro huo. Mwezi August mwaka 1941, mateso yalisambaa kote duniani na wayahudi kote barani Ulaya walikabiliwa na kuangamizwa, wakati huo London ikishambuliwa kwa mabomu na Bunge lake kupigwa na hivyo Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill na Rais wa Marekani Franklin D. Roosevelt wakaungana kujitolea kuweka maono ya kipekee kwa vizazi baada ya vita.  

Bwana Guterres anasema ahadi walizoziweka viongozi hao ambazo zilifahamika kama Mkataba wa Atlantic, ziliweka misingi ya mpangilio wa ulimwengu ulio wa haki zaidi, kwa kuzingatia haki ya watu wote kuchagua mfumo wao wa serikali na ushirikiano, haki za binadamu na utawala wa kisheria.  

“Miaka mitatu baadaye yaani mwaka 1945, kanuni nyingi na maadili ya Mkataba wa Atlantiki viliwekwa katika nyaraka yetu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa yaani Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Kwa njia nyingi, maono ya waanzilishi wetu yamethibitishwa. Hakujakuwa na Vita Ya Dunia ya tatu.” Ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  

Kikao cha Kwanza cha Baraza Kuu la ushirikiano wa mataifa (sasa Umoja wa Mataifa) Hii ni tarehe 10 January mwaka 1946 huko London, Uingereza.
UN /Marcel Bolomey
Kikao cha Kwanza cha Baraza Kuu la ushirikiano wa mataifa (sasa Umoja wa Mataifa) Hii ni tarehe 10 January mwaka 1946 huko London, Uingereza.

 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limefanya mengi 

Bwana Guterres ameeleza kuwa Baraza la Umoja wa Mataifa ambalo kwalo mataifa yamekuwa yakikutana kwa miaka 75 kujadili masuala muhimu, limeshuhudia nyakati nyingi za kihistoria.  

Guterres amesema, “kazi ya Baraza Kuu imesaidia kukuza afya ulimwenguni, kukuza elimu na viwango vya maisha, na kukuza haki za binadamu na usawa wa kijinsia.”  

Katibu Mkuu Wa Umoja wa Mataifa akirudi nyuma zaidi ameeleza kuwa azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu kuzipatia nchi uhuru katika mwaka 1960 ilikuwa ni hatua kubwa na tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, zaidi ya makoloni 80 yamepatiwa uhuru wake.  

Na kwa miaka ya hivi karibuni, Bwana Guterres amekumbusha namna ambavyo Umoja wa Mataifa umekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa COVID-19. Kwamba shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limeongoza kushughulikia afya na kuratibu vifaa muhimu, mafunzo na huduma.  

“Mwanzo mwa janga, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilichukua hatua haraka kupitisha  azimio la kutaka mshikamano wa ulimwengu kupambana na virusi.” Amesema Guterres.  

Na kushindwa nako kumekuwepo  

Bwana Guterres ameeleza kuwa pamoja na kujivunia mafanikio ya Umoja wa Mataifa lakini pia wanatambua kuwa kuna maeneo ambayo hawajafanya vizuri akitaja vitu kama mabadiliko ya tabianchi Akieleza kuwa namna dunia ambavyo imeshughulikia jambo hili si vya kutosha.  

“Muongo uliopita ulikuwa wenye joto zaidi katika historia ya bindamu. Viwango vya hewa ukaa viko katika kiwango cha juu. Moto na mafuriko, vimbunga na visulivuli vimekuwa hali ya kawaida.”  

Ameonyesha kuwa wanadamu wasipobadili mwenendo, “tunaweza kuelekea katika ongezeko hatari la joto zaidi ya nyuzi joto 3 katika karene hii. Na kwamba Bioanuwai inavunjika, viumbe milioni moja duniani viko hatarini kutoweka na mfumo wa ikolojia unatoweka mbele ya macho yetu.” 

Amesema katika nyakati za sasa, kumekuwa na vita ambazo inakuwa vigumu kuzitatu. Mivutano ya kijiografia inaongezeka na kuna tishio la nyuklia na makabiliano yamerejea. Pia ukosefu wa usawa unaongezeka, nja inaongezeka na idadi kubwa ya watu wameangukia katika umaskini uliokithiri kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kumi.  

Pia ameeleza namna COVID 19 ambavyo imeonesha uwepo wa pengo katika ushirikiano na mshikamano ulimwenguni. Ameeleza namna ambavyo suala la chanjo limeibua utaifa ambapo nchi tajiri zinashindana kununua chanjo kw ajili ya watu wao na kuwasahau watu waliko katika nchi maskini. Hata hivyo ameishukuru Uingereza kwa kuisaidia COVAX ambayo ilianzishwa na WHO ili inashughulika na kuhakikisha chanjo inapatikana kwa watu wote ulimwenguni.  

Bwana Guterres akijibu maswali ya washiriki kwa njia ya video  ametoa wito kwa ulimwengu mzima kuja pamoja na kuwa na mshikamano kushughulikia masuala yote ambayo hayako sawa ulimwenguni akitaja masuala kama kukosekana kwa usawa, mabadiliko ya tabianchi na mengine kama hayo.