Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano baina ya nchi za kusini umekuwa jawabu wakati huu wa COVID-19

Ushirika wa mataifa ya Kusini-SSC- umetoa mafunzo ya maelekezo kuhusu ulimaji wa mpunga Cote D'ivoire.
©FAO/Wang Jinbiao
Ushirika wa mataifa ya Kusini-SSC- umetoa mafunzo ya maelekezo kuhusu ulimaji wa mpunga Cote D'ivoire.

Ushirikiano baina ya nchi za kusini umekuwa jawabu wakati huu wa COVID-19

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Utashi wa ushirikiano baina ya nchi za kusini au zile zinazoendelea na mshikamano wa dunia bado uko hai ulimwenguni kote wakati huu ambapo tunahaha kukabiliana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya ushirikiano wa nchi za kusini hii leo.

 

Ingawa siku hii maadhimisho yake ni leo, Umoja wa Mataifa ulikuwa na tukio maalum lililofanyika siku ya Alhamisi ambapo maudhui yalikuwa njia kuelekea kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kupitia ushirikiano wa nchi za kusini hata baada ya janga la COVID-19.

Katibu Mkuu Guterres akasema kuwa nchi zinazoendelea zinasambaza vifaa vya matibabu, zinatoa msaada wa fedha na hata kubadilishana mbinu bora zaidi za jinsi ya kukabiliana na COVID-19 na ndio maana, “katika kuadhimisha siku hii tunaangazia uthabiti wa ushirikiano baina ya nchi za kusini katika kusongesha maendeleo endelevu hata nyakati za sasa za changamoto.”

Mshikamano na nchi za Kusini

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unatekeleza wajibu wake wa kuunga mkono ushirikiano baina ya nchi za kusini na ushirikiano wa utatu wakati wote huu wa janga la Corona ikiwemo kusongesha haraka msaada wa kifedha ili kusaidia mataifa hayo kuchukua hatua dhidi ya COVID-19 na hata katika hatua za kujikwamua baada ya janga hilo.

Kama mfano wa manufaa dhahiri ya ushirikiaon huo kupitia mfumo wa ushirikiano wa mataifa ya kusini, amekumbusha ukarabati wa hospitali pekee ya Barbduda ambayo iliharibiwa wakati wa kimbunga Irma kilichopiga ukanda wa Karibea mwaka 2017 akisema kuwa “hivi sasa imekarabatiwa na ina vifaa vyote vinavyotakiwa kusaidia jamii husika wakati huu wa janga la Corona.”

India na Honduras, kupitia ushirikiano wa nchi za kusini, SSC, zimekuwa zikifanya kazi pamoja kuimarisha matumizi ya vyanzo vyao vya nishati jadidifu.
UNDP Honduras
India na Honduras, kupitia ushirikiano wa nchi za kusini, SSC, zimekuwa zikifanya kazi pamoja kuimarisha matumizi ya vyanzo vyao vya nishati jadidifu.

Ushirikiano ni muhimu kuliko wakati wowote ule

Akiangazia ushirikiano hata baada ya janga la Corona, Katibu Mkuu amesema kuelekea kujikwamua vizuri, ushirikiano wa utatu kati ya nchi za kusini na jamii ya kimataifa utakuwa muhimu kuliko wakati wowote ule.
Amesihi kila mtu aratibu juhudi za kuongeza maendeleo ya ukanda wa kusini na kujenga mbinu bora za kujikwamua na hivyo kufanika SDGs ifikapo mwaka 2030.

Kufanikisha SDGs

Mapema Rais wa Baraza Kuu Tijjani Muhammad-Bande akizungumza kwenye tukio hlio kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa nchi za kusini katika muktadha wa muongo mmoja uliosalia kutekeleza malengo hayo amesema, “mwelekeo huu una wezo wa kuchangia katika kufanikisha malengo yetu ya kutokomeza umaskini, kutokomeza njaa, hatua kwa tabia nchi na ujumuishwa.”

Madhara ya virusi vya Corona

Wakati huu wa janga la Corona, ushirikiano baina ya nchi za kusini ni muhimu hasa wakat mataifa hayo yanapokabiliana na madhara ya kiuchumi na kijamii ya janga hilo.

COVID-19 imepanua wigo wa pengo la usawa ambalo tayari lilikuwepo, watu miioni 71 wanakadiriwa kutumbukia kwenye ufukara ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na wengine milioni 121 wanatarajiwa kuwa na lishe duni katika kipindi hicho hicho.

Ni kwa mantiki hiyo Bwana Muhammad-Bande amesisitiza umuhimu wa kujikita zaidi katika hatua mahsusi zitakazopunguza madhara ya ustawi na mbinu za watu kujipatia kipato hususan katika nchi hizo zinazoendelea.