UNHCR yaimarisha juhudi za kudhibiti COVID-19 miongoni mwa wakimbizi, Uganda 

3 Septemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake nchini Uganda wameimarisha juhudi za kudhibiti vifo na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 miongoni mwa wakimbizi wakati huu ambapo wakimbizi 89 tayari wameambukizwa ugonjwa huo, huku wawili wakiripotiwa kufariki dunia. 

Miongoni mwa hatua kubwa ambazo zimechukuliwa hivi karibuni ile ya 26 Agosti ambapo serikali ilitangaza upya vikwazo vyote vya kudhibiti COVID-19 katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali baada ya kifo kimoja kuthibitishwa na wengine 23 kuambukizwa. Vikwazo hivyo ni pamoja na kutotoka au kuingia kambini na kutekelezwa kwa amri ya kutotembea usiku kuanzia saa moja hadi kumi na mbili na nusu ambayo haitekelezwi sehemu zingine.

Bi. Leslie Velez, Mratibu mwandamizi wa mahusiano ya nje ya UNHCR Uganda amenieleza hali kote nchini, “Kyangwali kuna wagonjwa 23 ambao wanaendelea kupokea matibabu na kwa bahati mbaya mmoja alikufa ilipofikai pili Septemba na kujumlisha idadi ya mabukizi hadi 24 kambini. Kwa ujumla wakimbiiz 89 wamethibitishwa kwambukizwa kote nchini lakini 58 wametibiwa na kurejea aktika jamii zao. Jumla ya wafu kutokana na gonjwa hilo ni wakimbizi wawili”

Amehakikisha kuwa licha ya mlipuko huo kuathiri utoaji huduma katika jamii za wakimbizi, wanatumia kila mbinu kuona kwamba huduma zinaendelea kuwafikia hasa wale wenye mahitaji ya kipekee, “huduma muhimu za kuokoa maisha zinaendelela kutolewa. UNHCR, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali tuhakikisha msaada unatolewa kwa walio hatarini zaidi. Tarehe 24 Agosti UNHCR ilianza kusambaza vifaa kinga vya ziada  ili kuimarisha mbinu za kinga dhidi ya COVID-19 tukiwalenga wakimbizi laki moja na elfu ishirini”

Bi.Laslie amefichua kuwa hata wahudumu wa kibinadamu 44 wameambukizwa virusi vya corona tangu mlipuko wake nchini Uganda mnamo Machi.

Makaazi ya wakimbizi mengine ambayo yamesajili visa vya corona ni Adjumani, Parlorinya, Bidibidi, Palabek, Kiryandongo, Nakivale, Oruchinga and Kampala.

Kulingana na Laslie, UNHCR imeitikia hali hii pia kwa kusaidia wizara ya afya ya Uganda kuchunguza wakimbizi 27,167 na kuwezesha kupimwa kwa wengine 5,000 kuhusu hali yao ya COVID-19

Pia wanasaidia kuwezesha shughuli kwenye vituo 19 vya karantini kote nchini.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud