Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaongeza juhudu kunusuru maisha ya mamilioni Afrika dhidi ya COVID-19

Wakazi wa jimbo la Lagos waigiza kuhusu namna ya kukohoa kwenye kiwiko cha mkono wakati wa kampeni ya kuzuia virusi vya corona.
© UNICEF/Ojo
Wakazi wa jimbo la Lagos waigiza kuhusu namna ya kukohoa kwenye kiwiko cha mkono wakati wa kampeni ya kuzuia virusi vya corona.

UNHCR yaongeza juhudu kunusuru maisha ya mamilioni Afrika dhidi ya COVID-19

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linafanya kila juhudi kuhakikisha linanusuru maisha ya mamilioni ya watu ukanda wa Afrika Magharibi na Kati yaliyo hatarini kutokana na changamoto mpya iliyozuka ya virusi vya Corona au COVID-19.

Shirika hilo linasema nchi 21 za kanda hiyo ambazo nyingi zinakabiliwa na changamoto za vita, wakimbizi na wakimbizi wa ndani zinahitaji msaada ili kukabiliana na janga jipya linaloitikisa dunia hivi sasa.

COVID-19 imeongeza changamoto katika ukanda ambao tayari ni moja ya mgogoro mkubwa kabisa wa kibinadamu duniani ukihusisha zaidi ya watu milioni moja ambao wamelazimika kutawanywa.

Janga hili la corona kwa mujibu wa UNHCR limesababisha mipaka kufungwa na kuongeza shinikizo katika mifumo ya afya ambayo inayumba na uchumi dhaifu.

Moja ya vitu vinavyofanywa na shirika hilo la wakimbizi ni kuongeza msaada wa serikali kuweza kushughulikia hali ya kibinadamu inayozidi kuzorota. “Kipaumbele chetu ni kuhakikisha fursa ya usalama na kujaribu kupunguza athari za mlipuko wa janga hili la corona” limesema shirika hilo.

Hadi sasa nchi zote 21 za ukanda huo zimeripoti jumla ya wagonjwa 5000 wa COVID-19 na vifo Zaidi ya 100.

David ni mmoja wa viongozi wa jamii zinazowahifadhi wakimbizi katika makazi ya wakimbizi ya Adagom anasema “Hivi sasa tunapaswa kuwa waangalifu sana kuhusu COVID-19. Janga hili ni Dhahiri, na kwa hakika wametuwekea hadi ndoo hapa kwa ajili ya kunawa mikono na kuwa makini , pia hatupaswi kutoka nje , tunapaswa kusalia ndani kwenye maeneo ya kambi hadi pale mtakapoambiwa kwamba janga hili limekwisha.”

Na eneo hilo la Afrika Magharibi na Kati “ni moja ya eneo la Afrika leney idadi kubwa ya waliotawanywa likiwa na jumla ya wwakimbizi wa ndani milioni 5.6, wakimbizi milioni 1.3, watu waliorejea makwao milioni 1.4 ambao bado wanahitaji msaada na watu milioni 1.6 ambao hawana utaifa.”

UNHCR inasema kwa mfano Nigeria inahifadhi wakimbizi 57,000 n ashirika hilo linashirikiana kwa karibu na serikali na mamlaka ili kuimarisha fursa za huduma za afya , maji, usafi na vituo vya kujisafi hasa katika juhudi za kuwalinda wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.

Na kwa upande wa Niger UNHCR imetoa mafunzo kwa wasanii na mafunzi cherahani ili kutengeneza barakoa kwa ajili ya wakimbizi na watu wa jamii zinazowahifadhi.