Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango ya kudhibiti COVID-19 ilianza punde tu baada ya maambukizi kuripotiwa China, yasema Mauritius

Mtu anayeugua magonjwa ya njia ya hewa anashauriwa kuvaa barakoa kama aonekanavyo mwanamke huyu pichani,
Unsplash/Michael Amadeus
Mtu anayeugua magonjwa ya njia ya hewa anashauriwa kuvaa barakoa kama aonekanavyo mwanamke huyu pichani,

Mipango ya kudhibiti COVID-19 ilianza punde tu baada ya maambukizi kuripotiwa China, yasema Mauritius

Afya

Mauritius, taifa la kisiwani lililo katika bahari ya Hindi limeelezea kile kilicholiwezesha kudhibiti ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 punde tu baada ya kuthibitishwa kuwepo kwa wagonjwa 3 nchini humo mwezi Machi mwaka huu.

Hivi sasa maisha yamerejea katika hali ya kawaida ingawa wananchi bado wanachukua hatua za kujikinga kwa kuvaa barakoa baada ya mafanikio makubwa ya kudhibiti COVID-19. 

Tangu ugonjwa huo ubainike tarehe 18 mwezi Machi mwaka huu hadi leo hii idadi ya wagonjwa waliothibtishwa ni 346 ambapo kati yao hao ni 10 ndio wamefariki dunia. 

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO linasema kuwa, tangu tarehe 26 mwezi Aprili mwaka huu hakuna maambukizi yoyote mapya ya ndani nchini Mauritius yameripotiwa, je nini siri ya kisiwa hiki? Dkt. Vasantrao Gujadhur ni Mkurugenzi wa Afya nchini humo na anasema kuwa, “unafahamu tangu kutangazwa mlipuko wa COVID-19 nchini China mwezi Januari mwaka huu, kazi ilianza hapa. Kati ya tarehe 15 na 16 Januari tulishakuwa na mipango ya nini cha kufanya. Tulianza kuelimisha wananchi kupitia redio, televisheni, mabango na pia kuhamaisha kuhusu dalili na njia za kujikinga na COVID-19. Pia nini wafanye iwapo wakiona dalili. Hii ilifanyika kila siku kuhakikisha inawaingia kwenye fikra zao.” 

Uzoefu wa kufuatilia wagonjwa kupitia magonjwa ya milipuko kama vile denge na surua ulitumika katika COVID-19 na serikali iliimarisha mipango ya ufuatiliaji waambata wa wagonjwa. 

Mwongozo wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa ,WHO wa usimamizi na uchunguzi wa wasafiri katika vituo vya kuingilia nchini Mauritius na uwekaji wa vituo vya karantini ulizingatiwa kuhusu serikali ikichukua hatua za kisera. WHO pia ilisaidia kwenye upatikanaji wa vifaa na maabara. 

Dkt. Laurent Musango ni mwakilishi wa WHO nchini Mauritius na anasema kuwa, “tulianza kwa kufafanua mpango wa kitaifa wa kujiandaa na kuchukua hatua dhidi ya mlipuko. Na hii ilifanyika kwa msaada wa WHO. Na hatua za utekelezaji zilizingatia misingi mizuri inayopendekezwa na WHO.” 

Punde tu baada ya kupatikana kwa wagonjwa watatu wa kwanza tarehe 18 mwezi Machi mwaka 2020, Mauritius ilichukua hatua za kijasiri za kuzuia watu kuwa nje ya makazi yao kwa muda fulani ili kudhibiti kuenea kwa gonjwa hilo hatari.