Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 inahimiza ubunifu wa kiafya barani Afrika-WHO

Kijana Tanzania atengeneza ndoo ya kunawa mikono bila kugusa koki wala sabuni.
UN News/ UNIC Tanzania
Kijana Tanzania atengeneza ndoo ya kunawa mikono bila kugusa koki wala sabuni.

COVID-19 inahimiza ubunifu wa kiafya barani Afrika-WHO

Afya

Utafiti mpya wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO uliotangazwa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, Brazzaville, umesema janga la COVID-19 limeongeza nguvu kwenye maendeleo ya ubunifu zaidi ya 120 wa teknolojia ya afya ambao umejaribiwa au kupitishwa barani Afrika.

Dr Matshidiso Moeti, ambaye ni Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika katika hotuba yake ya ufunguzi amesema, "Utafiti wa teknolojia mpya 1000 au zilizofanyiwa marekebisho marekebisho ambazo zimetengenezwa ulimwenguni kulenga maeneo tofauti ya kushughulikia COVID-19 inagundua kuwa Afrika inachangia asilimia 12.8 ya ubunifu. Sehemu za kushughulikia ni pamoja na ufuatiliaji, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa, ushiriki wa jamii, matibabu, mifumo ya maabara na maambukizi, kinga na udhibiti. ” 

Aidha, yaliyomo katika utafiti yakithibitishwa na Dkt Moet ni kwamba barani Afrika, asilimia 57.8 za ubunifu wa kupambana na COVID-19 ulishawishiwa na teknolojia ya mawasiliano, asilimia 25 ikitegemea katika uchapishaji wa mfumo wa 3D na asilimia 10.9 ukiwa ubunifu wa roboti. Mathalani kwa upande wa teknolojia ya mawasiliano, Afrika Kusini imekuja na mfumo ambao unatumia WhatsApp kuwasiliana, Angola kuna vifaa vya mgonjwa kujipima, Ghana kuna Apu za kufuatilia wagonjwa na watu waliokutana nao na vifaa vya taarifa nchini Nigeria. WHO inasema nchi ambazo zimeonesha ubunifu zaidi wakati wa COVID-19 ni Afrika Kusini kwa asilimia 13, Kenya asilimia 10, Nigeria asilimia 8 na Rwanda asilimia 6. 

Dr Moet akisifia namna vijana wa Afrika walivyojitosa katika ubunifu wa kupambana na COVID-19 amesema ni vyema kuona nguvu za ujana za bara zima zinawaka moto kupambana na COVID-19 kisha akaongeza. "COVID-19 ni mojawapo ya changamoto kubwa za kiafya katika kizazi hiki, lakini pia ni fursa ya kusukuma mbele uvumbuzi, uhalisia na ujasiriamali katika teknolojia za kuokoa maisha," 

Kwa mujibu wa shirika la afya kwa nchi za America, PAHO kwa namna uchumi ulivyoendelea zaidi ndivyo unavyozidi kuvumbua na kinyume chake, lakini uchumi mwingine unavunja muundo huu kwa kufanya vizuri au vibaya kuliko ilivyotabiriwa. Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ndio eneo lenye idadi kubwa ya uchumi inayofanya vizuri kuliko matarajio ikilinganishwa na kiwango chao cha maendeleo. Ingawa hii inatia moyo, WHO inasema uwekezaji ni muhimu ili kuzidisha ubunifu katika Afrika. Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia unaripoti kuwa nchi za Kiafrika, zinawekeza kidogo katika uvumbuzi kuliko nchi zilizoendelea na bara halifanyi vizuri kulinganisha na uwezo wake.