Wahudumu wa kibinadamu ni mashujaa wanaoweka rehani maisha yao ili kuokoa ya wengine:Guterres

19 Agosti 2020

Ikiwa leo ni siku ya huduma za kibinadamu duniani Umoja wa Mataifa umesema unawaenzi wahudumu hao ambao wanakabiliana na changamoto lukuki katika kuokoa na kuboresha maisha ya mamilioni ya watu. 

Kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “wahudumu hawa ni mashujaa wa kweli na wanafanya maajabu katika nyakati ngumu ili kusaidia wanawake, wanaume na watoto ambao maisha yao yamesambaratishwa na majanga.”

Ameongeza kuwa mwaka huu wahudumu wa kibinadamu wamelemewa kuliko wakati mwingine wowote “Wanakabiliana na janga la kimataifa la COVID-19 ambalo limesababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya kibinadamu kutokana na athari zake. Kupoteza ajira, elimu, chakula, maji na usalama vinawasukuma mamilioni ya watu katika hali mbaya.” 

Katibu mkuu amesema vikwazo vya kusafiri ili kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona vinamaanisha kwamba jamii, asasi za kiraia na mashirika ya kijamii kugeuka kuwa wahudumu wa kwanza kuliko ilivyokuwa awali. 

Na kwa mantiki hiyo Guterres amesema “Mwaka huu tunawasherehekea wao, watu ambao mara kwa mara wana mahitaji yao, kama vile wakimbizi kuzisaidia jamii zinazowahifadhi, wahudumu wa afya ambao wanawahudumia wagonjwa na kutoa chanjo kwa watoto na wahudumu wa kibinadamu ambao wanajadili kupata fursa katika maeneo ya vita ili kufikisha chakula, maji na madawa. Ni mashujaa wasiotarajiwa wa kukabiliana na janga hili na mara nyingi wanaweka rehani maisha yao ili kuokoa yaw engine.” 

Katibu Mkuu ametoa wito kwa dunia kuungana naye katika siku hii ili kutoa shukran na msaada kwa wahudumu hao jasiri wa kibinadamu, wahudumu wa afya na wato hudumu ya kwanza ambao wanaonyesha mshikamano na utu katika wakati huu wenye mahitaji makubwa yasiyotarajiwa. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter