Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko watoa huduma kwa kuweka rehani maisha yenu kwa maslahi ya wengi- UNHCR

Mfanyakazi wa huduma za kibinadamu akimsaidia mkimbizi wa Syria mwenye ulemavu ambaye mguu wake ulikatwa kutokana na ugonjwa wa kisukari. Hapa walikuwa wanavuka eneo lililopo kati ya Macedonia na Serbia
Jodi Hilton/IRIN

Msaada wa Kibinadamu

Hebu fikiria maisha ya walio kwenye mizozo kuanzia barani Afrika, Asia, Ulaya hadi Amerika yangalikuwa vipi bila watoa misaada ya kibinadamu wanaoweka rehani uhai wao?

Hivyo ndivyo anahoji Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi wakati akizungumza mjini Geneva, Uswisi hii leo, kuelekea siku ya watoa  huduma za misaada duniani tarehe 19 mwezi huu.

Bwana Grandi amesema watoa huduma za misaada walio jasiri huweka hatarini maisha  yao ili kulinda watu walio hatarini zaidi duaniani kote na “mamuzi yao magumu wanayochukua ili kwenda maeneo magumu zaidi. Kila wakati ni wito wa uamuzi kati ya uhai na kifo.”

Amesisitiza azma ya UNHCR ya kuendelea kuunga mkono kwa uthabiti jitihada za pamoja za mashirika ya kibinadamu na azma ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi wa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye maeneo hatari.

Wafanyakazi wa huduma za kibinadamu kutoka shirika linalofanya kazi pamoja na UNHCR wakisaidia watu waliowasili Yemen kwa njia ya bahari.
SHS/UNHCR
Wafanyakazi wa huduma za kibinadamu kutoka shirika linalofanya kazi pamoja na UNHCR wakisaidia watu waliowasili Yemen kwa njia ya bahari.

Hebu fikiria maisha ya walio kwenye mizozo kuanzia barani Afrika, Asia, Ulaya hadi Amerika yangalikuwa vipi bila watoa misaada ya kibinadamu wanaoweka rehani uhai wao?

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2017, jumla ya watoa huduma za kibinadamu 179 waliuawa, ambapo idadi kubwa ilikuwa Sudan Kusini, Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria na Bangladesh. Watumishi wengine zaidi ya 300 walilengwa kwa mashambulizi, ubakaji au kutekwa nyara.

 “Ingawa napata ahueni kuwa hakuna mfanyakazi wa UNHCR aliyepoteza maisha yake akiwa kazini, bado nasalia na hofu juu ya idadi kubwa ya matukio ya kiusalama yanayoathiri wafanyakazi wenzetu wa UNHCR,” amesema bwana Grandi.

Kamishna Grandi amesema mazingira ya usalama yanazidi kuwa na changamoto, lakini amesema uelewa juu ya kuzingatia masharti ya usalama unazidi kuongezeka miongoni mwa watendaji hao.

Amepongeza kazi inayofanywa na kitengo cha usalama cha shirika hilo kilichoanzishwa miaka 25 iliyopita.

Siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa kibinadamu ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2008 kuenzi watendaji wa chombo hicho waliouawa wakati wa mashambulizi dhidi ya makao makuu ya UN huko Baghdad, Iraq mwaka 2005.

Miongoni mwao ni aliyewahi kuwa afisa mwandamizi wa UNHCR Sergio Vieira de Mello.