Siku ya huduma za kibinadamu yamulika wanawake waliojitolea kusaidia wengine mizozoni

19 Agosti 2019

Leo ni siku ya huduma za kibinadamu duniani ambapo Umoja wa Mataifa unapigia chepuo mwaka huu wanawake waliojikita katika kutoa huduma za kibinadamu kote ulimwenguni.

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wanawake wanamulikwa kutokana na tofauti kubwa wanayoleta pale wanaposhiriki kutoa  huduma za kibinadamu kwa mamilioni ya wanawake, wanaume na watoto.

“Kuanzia kuwasaidia raia waliokumbwa na migogoro hadi kushughulikia milipuko ya magonjwa, wanawake wahudumu wa kibinadamu wako mstari wa mbele. Uwepo wao unafanya operesheni za misaada kuwa nzuri zaidi kwa kuongeza ufikiaji wao. Pia unaboresha hatua zinazochukuliwa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, ambao huongezeka wakati wa dharura,” amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu ametaka kila mtu kushiri katika simulizi za wanawake hao, simulizi ambazo zina nguvu na hivyo “kuthibitisha ahadi yetu  ya kuimarisha jukumu la wanawake katika operesheni za kibinadamu.”

Kupitia ujumbe huo Katibu Mkuu Guterres amewageukia pia viongozi wa dunia na pande katika mizozo akisema kuwa wanapaswa kuhakikisha kwamba wahudumu wa kibinadamu wanalindwa dhidi ya madhara, kama inavyotakiwa  chini ya sheria za kimataifa.

“Ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu unaendelea duniani kote. Ni lazima uchunguzwe na kuchukuliwa hatua,” amesema Bwana Guterres huku akitamatisha ujumbe wake akisema kuwa “katika siku ya huduma za Kibinadamu na kila siku, tunasimama pamoja na wahudumu wa kibinadamu kote duniani.”

Siku ya huduma za kibinadamu duniani huadhimishwa kila tarehe 19 mwezi Agosti kila mwaka tangu mwaka 2008 kukumbuka shambulizi dhidi ya jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad nchini Iraq tarehe 19 Agosti mwaka 2003.

Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 22 akiwemo mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq Sergio Vieira de Mello.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuadhimisha siku hii mwaka 2008 kupigia chepuo ulinzi na usalama wa wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu sambamba na utu wao kwenye maeneo yenye mizozo.

Tukio la kuweka shada la maua kuadhimisha siku ya huduma za kibinadamu duniani. Pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed, (wa pili kushoto) na Mwakilishi wa kudumu wa Iraq kwenye Umoja wa Mataifa (wa kwanza kushoto)
UN /Loey Felipe
Tukio la kuweka shada la maua kuadhimisha siku ya huduma za kibinadamu duniani. Pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed, (wa pili kushoto) na Mwakilishi wa kudumu wa Iraq kwenye Umoja wa Mataifa (wa kwanza kushoto)

Makao Makuu ya UN New York, Marekani kwafanyika tukio maalum

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed ameongoza tukio la kukumbuka wale waliopoteza maisha mjini Baghdad, Iraq tarehe 19 mwezi Agosti mwaka 2003 sambamba na kutambua mchango wa maelfu ya wanawake wanaofanya kazi za kujitolea kusaidia binadamu walio hatarini.

Katika shambulio hilo mjini Baghdad watu 22 waliuawa akiwemo Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Sergio Vieira de Mello.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Bi. Mohammed amesema, “wale wanaoshambulia Umoja wa Mataifa wanataka tuwe na uoga, tujione dhaifu na turudi nyuma. Mchango wa wale waliopoteza maisha ndio bado upo na ndio maana tunaahidi kuokoa watu kutoka kwenye shida na vifo na azma yetu ya kujenga mustakabali bora kwa wote.”

Katika tukio hilo, washiriki walinyamaza kimya kwa dakika moja kukumbuka waliopoteza maisha wakihudumia binadamu.

Duniani kote kuna wanawake wahudumu wa kibinadamu 250,000 idadi ambayo ni zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi katika sekta ya huduma za kibinadamu.

Licha ya umuhimu wa kazi hiyo, bado ni kazi hatari zaidi duniani.

Tangu mwezi Agosti mwaka 2003, zaidi ya wafanyakazi 4,500 wa huduma za kibinadamu wameuawa, au wamejeruhiwa au hata kushambuliwa na kushikilwa kinyume cha sheria wakati wakiwa kazini.

Umoja wa Mataifa unasema wahudumu wa kibinadamu wanawake wako hatarini zaidi kuporwa, kufanyika ukatili wa kingono na ghasia nyingine.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter