Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule zikiwa zinaanza kufunguliwa, bado hakuna huduma za kujisafi kujikinga na COVID-19- Ripoti

Mwanafunzi wa kike nchini Ghana akinawa mikono kwa sabuni kabla ya kurejea darasani ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha elimu inaendelea huku wakidhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
UNICEF/Geoffrey Buta
Mwanafunzi wa kike nchini Ghana akinawa mikono kwa sabuni kabla ya kurejea darasani ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha elimu inaendelea huku wakidhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Shule zikiwa zinaanza kufunguliwa, bado hakuna huduma za kujisafi kujikinga na COVID-19- Ripoti

Afya

Wakati huu ambapo shule katika maeneo mbalimbali duniani zikihaha kuanza tena mihula mipya baada ya karantini kutokana na janga la virusi vya Corona au COVID-19, ripoti mpya ya mashirika ya Umoja wa Mataifa imeonesha kuwa asilimia 43 ya shule kote ulimwenguni mwaka 2019 hazikuwa na huduma za msingi za kujisafi, ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, sharti ambalo ni la msingi kwa shule kuweza kuwa na mazingira salama kwa wanafunzi wakati huu wa janga la COVID-19.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na New York, Marekani na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, na lile la kuhudumia watoto UNICEF imesema kuwa kiwango hicho ni sawa na shule 2 kati ya shule 5 zilizotafitiwa. 

Kwa mujibu wa ripoti, watoto milioni 818 hawana huduma za msingi za kujisafi shuleni, hali inayowaweka hatarini kupata Corona na magonjwa mengine ya kuambukiza. 

“Zaidi ya theluthi moja ya idadi hiyo wako nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na idadi ya shule zisizo na huduma za kuna mikono ni 7 kati ya 10 na nusu ya hizo hazina huduma za msingi za kujisafi na huduma za maji,” imesema ripoti hiyo. 

Wasichana wa shule huko Cambodia wakiosha mikono yao kwa kutumia maji kutoka kwa kituo cha shule cha WASH.
© UNICEF/Bona Khoy
Wasichana wa shule huko Cambodia wakiosha mikono yao kwa kutumia maji kutoka kwa kituo cha shule cha WASH.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema kuwa, “kufungwa kwa shule kote duniani tangu kuingia kwa COVID-19 kumesababisha changamoto za kipekee kwa elimu na ustawi wa watoto. lazima tupatie kipaumbele watoto kujifunza. Hii ina maana kuhakikisha shule ni salama pindi zinapofunguliwa, ikiwemo usafi wa mikono, maji safi na salama ya kunywa na huduma za kujisafi.” 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, “kupata huduma za maji safi, kujisafi na usafi ni muhimu katika kudhibiti maambukizi maeneo yote ikiwemo shuleni. Ni lazima kiwe kipaumbele cha serikali katika mkakati wake wa kufungua na kuendesha shule kwa usalama wakati huu wa janga la COVID-19 duniani.” 

Ripoti inasisitiza kuwa serikali zinazotaka kudhibiti kuenea kwa COVID-19 lazima ziweke mizania juu ya umuhimu wa kutekeleza mikakati ya afya ya umma na madhara kiuchumi na kijamii yatokanayo na mikakati ya kuzuia kuchangamana. 

Ripoti inataja mambo ya kuzingatia wakati watoto wakirejea shuleni kwa kutumia miongozo iliyotolewa na UNESCO, UNICEF, WFP na Benki ya Dunia kwa ushauri kutoka mamlaka za kitaifa na kimkoa. 

Miongozo hiyo inahusisha kuwepo kwa kanuni za huduma za kujisafi au WASH, matumizi ya vifaa vya kujikinga dhidi ya Corona, kunawa na kutakasa mikono na maeneo, vituo vya kunawa mikono kwa maji na sabuni na vyoo visafi.