Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO, UNICEF zataka shule zifunguliwe kwa njia salama Afrika

Mwanafunzi wa shule ya msingi akisoma nyumbani kwao Kibera, Kenya.
© UNICEF/Brian Otieno
Mwanafunzi wa shule ya msingi akisoma nyumbani kwao Kibera, Kenya.

WHO, UNICEF zataka shule zifunguliwe kwa njia salama Afrika

Utamaduni na Elimu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la afya WHO na la kuhudumia watoto UNICEF yamesema hatua ya shule kufungwa kwa muda mrefu kwa lengo la kuwalinda wanafunzi na virus vya corona au COVID-19 inawaumiza wanafunzi hao kwa njia nyingine na wamezitaka serikali barani Afrika kuchaguza ufuanguaji salama wa shule huku zikichukua hatua kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo. 

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya mashirika hayo iliyotolewa leo mjini Brazzaville , utafiti uliofanywa na WHO katika nchi 39 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara umebaini kwamba shule zimefunguliwa kikamilifu katika nchi sita pekee, zimefungwa katika nchi 14 na zimefunguliwa kwa ajili ya mitihani tu katika nchi 19 zingine. 

Na takriban katika nchi 12 kuna mipango ya kuanza masomo tena mwezi Septemba ambao ni msimu wa kufungua shule katika nchi nyingi. 

Hata hivyo UNICEF na WHO wamesema “Athari za kuingilia elimu kwa muda mrefu ni kubwa pamoja na mambo mengine zinajumuisha lishe duni, msongo wa mawazo, ongezeko la watoto kushuhudia ukatili na unyanyasaji, mimba za utotoni na changamoto za jumla za maendeleo ya akili kwa watoto kutokana na kushuka kwa kiwango cha watoto kuchangamana kwa sababu ya kufunga shule.” 

Msichana mwanafunzi wa Ethiopia anasomea nyumbani wakati ambapo shule zimefungwa kuzuia kusambaa kwa COVID-19.
© UNICEF/NahomTesfaye
Msichana mwanafunzi wa Ethiopia anasomea nyumbani wakati ambapo shule zimefungwa kuzuia kusambaa kwa COVID-19.

Kwa upande wa Mashariki na Kusini mwa Afrika UNICEF imebaini kwamba kiwango cha ukatili kwa watoto kimeongezeka, huku kiwango cha lishe kikishuka kwa sababu ya watoto zaidi ya milioni 10 kukosa mlo shuleni. 

Na kwa upande wa wasichana taarifa hiyo imesema hususan wale waliotawanywa au wanaoishi katika kaya za kipato cha chini hatari inayowakabili ni kubwa zaidi, kwa mfano kufungwa kwa shule mwaka 2014 Afrika Magharibi kufuatia mlipuko wa Ebola, kulisababisha idadi ya mimba kwa wasichana vigori nchini Sierra Leone kuongezeka mara mbili na wasichana wengi walishindwa kuendelea na masomo shule zilipofunguliwa.

WHO na UNICEF wanasema athari za muda mrefu za kijamii na kiuchumi za kuendelea kufungwa shule zinatia hofu kwani kwa mujibu wa Benki ya Dunia zitaweza kusababisha hasara ya mapato ya dola  4,500 kwa kila mtoto na kiwango kinaweza kuwa kikubwa zaidi kwa wazazi wanaolazimika kusalia nyumbani kuangalia watoto kwa kushindwa kumudu malipo ya huduma za kuela watoto kwenye vituo. 

Mkurugenzi wa WHO Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “Shule zimefungua mlango wa mafanikio kwa Waafrika wengi, pia shule zimetoa maskani salama kwa watoto wengi wakati wa mazingira yenye changamoto. Tusifumbwe macho na juhudi zetu za kupambana na COVID-19 na tukaishia kupoteza kizazi hiki. Kama nchi zinavyorejea katika kazi na biashara zake kwa usalama , tunaweza kufungua shule. Na uamuzi huu uende sanjari na muongozo wa kufuatilia hatari na kuhakikisha usalama wa watoto, waalimu na wazazi kwa kuzingatia mambo muhimu ya kujitenga.”