Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benjamin William Mkapa alikuwa mwanadiplomasia mmbobevu na mpenda amani- Guterres 

Benjamin Mkapa, (katikati mwenye tai) akifuatilia uandikishaji wa wapiga kura ya maoni Sudan Kusini kabla ya upigaji kura wenyewe. Picha hii ni ya 16 Novema 2010.
UN Photo/Tim McKulka
Benjamin Mkapa, (katikati mwenye tai) akifuatilia uandikishaji wa wapiga kura ya maoni Sudan Kusini kabla ya upigaji kura wenyewe. Picha hii ni ya 16 Novema 2010.

Benjamin William Mkapa alikuwa mwanadiplomasia mmbobevu na mpenda amani- Guterres 

Masuala ya UM

Kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin William Mkapa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayati Mkapa alikuwa mwanadiplomasia mbobevu na mpigania amani anayeheshimika ambaye alihamasisha maridhiano.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York ameeleza kuwa na masikitiko makubwa baada ya kufahamu kuhusu kifo cha Benjamin William Mkapa.  

“Katika wakati huu wa majonzi, Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia ya Rais huyo wa zamani  pamoja na serikali na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.  

Aidha Bwana Guterres ameenda mbali zaidi na kueleza kuwa, “Benjamin William Mkapa alikuwa chombo muhimu katika kuwezesha mazungumzo ya Burundi yaliyoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya uongozi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na alikuwa  sehemu ya jopo viongozi wa Muungano wa Afrika lililosimamia makubaliano kufuatia kutokuelewa katika uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 hadi 2008.”

Tweet URL

 

Hayati Benjamin William Mkapa pia alikuwa mjumbe wa jopo la watu mashuhuri lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya tathimini Alikuwa pia mwanachama wa Jopo la watu wanaojulikana aliyeteuliwa na Katibu Mkuu kukagua na kuboresha jukumu la kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD.   

Rais wa Baraza Kuu la UN naye apaza sauti

Wakati huo huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Profesa Tijjani Muhammad-Bande , kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, "nimehuzunishwa na taarifa ya kwanza Benjamin Mkapa, Rais wa zamani wa Tanzania amefariki dunia. Mheshimiwa Mkapa alikuwa bingwa asiyechoka wa amani na demokrasia kwenye ukanda wa Afrika.  Salamu zangu za dhati za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Tanzania. Mchango wake katu hautosahaulika."