Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania amefariki dunia

Rais Benjamin Mkapa akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Septemba 2004 jijini New York, Marekani.
UN /Michelle Poiré
Rais Benjamin Mkapa akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Septemba 2004 jijini New York, Marekani.

Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania amefariki dunia

Masuala ya UM

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa amefariki dunia leo, akiwa na umri wa miaka 81.
Taarifa za kifo chake zimetangazwa kwa taifa usiku wa kuamkia leo Ijumaa kupitia televisheni na Rais John Magufuli kutokea mji mkuu Dodoma.

Katika taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema, “ndugu zangu watanzania, habari za jioni na habari za usiku. Usiku wa kuamkia leo kwa sababu sasa ni saa 6 karibu na dakika 25,  kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa. Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya Tatu, amefariki. Amefariki kwenye hospitali Dar es salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe watanzania tulipokee hili na tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea mzee wetu, Rais mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele ya haki. Taarif azinigne zitaendelea kutolewa lakini Mzee Mkapa hatunaye tena, asanteni sana.” 
Kufuatia kifo hicho, serikali ya Tanzania imetangaza siku 7 za maombolezo ambapo bendera itapepea nusu mlingoti.
Rais mstaafu Mkapa ambaye alizaliwa tarehe 12 Novemba mwaka 1938 alishika nyadhifa hiyo kubwa zaidi Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005 baada ya kumaliza awamu zake mbili za uongozi, ambapo kila awamu ni miaka 5.

Mkapa na Umoja wa Mataifa

Kwa Umoja wa Mataifa, hayati Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake katika diplomasia ya kuleta amani, hususan baada ya kustaafu.

Tarehe 21 mwezi Septemba mwaka 2010, aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Ban Ki-Moon kuongoza jopo la kusimamia kura ya maoni ya kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka Sudan.

Mkapa akiongozana na wajumbe ambao ni Antonio Monteiro, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ureno na Bhoiraj Pokharel, Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Uchaguzi nchini Nepal, walitembelea mara kadhaa Sudan kuhakikisha ufanikishaji wa kura hiyo ya maoni.

Halikadhalika alikuwa akihutubia vikao vya Baraza  la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mwelekeo wa kura hiyo ya maoni.

Benjamin William Mkapa akizungumza na waandishi wa habari tarehe 16 Desemba 2010 baada ya kuhutubia Baraza la Usalama kuhusu kura ya maoni Sudan Kusini  ambako yeye alikuwa Mwenyekiti wa jopo la usimamizi.
UN Photo/JC McIlwaine
Benjamin William Mkapa akizungumza na waandishi wa habari tarehe 16 Desemba 2010 baada ya kuhutubia Baraza la Usalama kuhusu kura ya maoni Sudan Kusini ambako yeye alikuwa Mwenyekiti wa jopo la usimamizi.

Katika moja ya mikutano na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum mwezi Desemba mwaka 2010 uliokuwa na lengo la kufanikisha kura hiyo ya maoni,  Mkapa alisema kuwa, “uwazi wa jinsi kura hizo zinahesabiwa na matokeo yanakokotolewa pia ni muhimu sana. Matokeo yanapaswa kutangazwa kwa uwajibikaji mkubwa.”

Kura ya maoni ya Sudan Kusini kujitenga kutoka Sudan ilifanyika kuanzia tarehe 9 hadi 15 Januari mwaka 2011 na matokeo ya kura hiyo yalidhihirisha nia ya Sudan Kusini kujitenga na hatimaye ikapata uhuru tarehe 9 Julai mwaka 2011.

Mkapa na Burundi

Kutokana na uwezo wake wa diplomasia ya usuluhishi, Mkapa ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania aliteuliwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, jukumu ambalo lilimpatia pia fursa ya kukutana na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres mwezi Februari mwaka 2019 kumpatia hatua zilizofikiwa wakati huo ambapo Burundi ilikuwa inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu mwaka 2020.