Kifo cha Rais mstaafu Mkapa si pigo tu kwa Tanzania, bali pia kwa jumuiya ya kimataifa:Balozi Gastorn 

24 Julai 2020

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn amesema kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia leo jijini Dar es salaam sio pigo kwa Tanzania tu bali kwa jumuiya nzima ya kimataifa. 

Balozi Gastorn amesema kuwa hayati Mkapa alikuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia nguli na tayari salamu za rambirambi kufutia msiba wake zinaendelea kumiminika kutoka kwa balozi za nchi mbalimbaki kwenye Umoja wa Mataifa na kwa Katibu Mkuu Antonio Guterres“Hapa kwenye Umoja wa Mataifa tumepokea tarifa za msiba wa Muheshimiwa Benjamin William Mkapa Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mshituko mkubwa sana. Hakika ni pigo kubwa sana kwa taifa letu, kwa bara la Afrika na kwa Dunia nzima kwa ujumla. Alipokuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania alikuwa mwenyekiti wa kampeni katika Umoja wa Mataifa zilizofanikisha kumchagua Dkt. Salim Ahmed Salim wa Tanzania kuwa Rais wa 34 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1979 hadi mwaka 1980. '

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa akifuatilia upigaji kura ya maoni kwa wananchi wa Sudan Kusini kujitenga na Sudan. hii ilikuwa tarehe 9 Januari 2011.
UN /Tim McKulka
Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa akifuatilia upigaji kura ya maoni kwa wananchi wa Sudan Kusini kujitenga na Sudan. hii ilikuwa tarehe 9 Januari 2011.

Balozi Gastorn ameongeza kuwa , "Hayati Mkapa akiwa madarakani na baada ya kustaafu amefanya mambo mengi makubwa ya kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa. Mwaka 2005 chini ya uongozi wake Tanzania ilichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mwaka 2003 hadi mwaka 2004 alikuwa mwenyekiti mwenza wa kamati ya utandawazi na jamii. Alitoa mchango mkubwa katika kuleta amani na usalama kwenye nchi za maziwa makuu, alikuwa ni mjumbe katika kamati ya usuluhishi katika mgogoro wa kisiasa nchini Kenya na hata kuweza kufanikisha uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Aliongoza kwa mafanikio jopo la Umoja wa Mataifa kuhakikisha matakwa na haki ya nchi inaheshimika katika kura ya maoni kule Sudan ya kusini na katika jimbo la Abyei. "

Rais John Magufuli atangazia umma kifo cha Rais mstaafu Mkapa

Taarifa za kifo cha Mkapa zilitangazwa na Rais wa Tanzania John Magufuli kupitia televisheni. "ndugu zangu watanzania, habari za jioni na habari za usiku. Usiku wa kuamkia leo kwa sababu sasa ni saa 6 karibu na dakika 25,  kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa. Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya Tatu, amefariki. Amefariki kwenye hospitali Dar es salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe watanzania tulipokee hili na tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea mzee wetu, Rais mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele ya haki. Taarifa  nyingine zitaendelea kutolewa lakini Mzee Mkapa hatunaye tena, asanteni sana.”

Hakika Taifa limepoteza nguzo imara. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,  Dkt. John Magufuli - Rais wa Tanzania

Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter pia amesema pamoja na kusikitishwa na kifo cha Mkapa, atamkumbuka kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi akisema kuwa, “hakika Taifa limepoteza nguzo imara. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,”

Tayari serikali ya Tanzania imetangaza siku 7 za maombolezo ambapo bendera itapepea nusu mlingoti.

Rais mstaafu Mkapa ambaye alizaliwa tarehe 12 Novemba mwaka 1938 alishika nyadhifa hiyo kubwa zaidi Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005 baada ya kumaliza awamu zake mbili za uongozi, ambapo kila awamu ni miaka 5.

Mkapa na Umoja wa Mataifa

Kwa Umoja wa Mataifa, hayati Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake katika diplomasia ya kuleta amani, hususan baada ya kustaafu.

Kutoka kulia :Benjamin Mkapa, António Monteiro, na Bhojraj Pokharel wajumbe wa jopo la Katibu Mkuu kuhusu Sudan
NAMS
Kutoka kulia :Benjamin Mkapa, António Monteiro, na Bhojraj Pokharel wajumbe wa jopo la Katibu Mkuu kuhusu Sudan

Tarehe 21 mwezi Septemba mwaka 2010, aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Ban Ki-Moon kuongoza jopo la kusimamia kura ya maoni ya kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka Sudan.

Katika moja ya mikutano na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum mwezi Desemba mwaka 2010 uliokuwa na lengo la kufanikisha kura hiyo ya maoni,  Mkapa alisema kuwa,“Uwazi wa jinsi kura hizo zinahesabiwa na matokeo yanakokotolewa pia ni muhimu sana. Matokeo yanapaswa kutangazwa kwa uwajibikaji mkubwa.”

Kura ya maoni ya Sudan Kusini kujitenga kutoka Sudan ilifanyika kuanzia tarehe 9 hadi 15 Januari mwaka 2011 na matokeo ya kura hiyo yalidhihirisha nia ya Sudan Kusini kujitenga na hatimaye ikapata uhuru tarehe 9 Julai mwaka 2011.

Kutokana na uwezo wake wa diplomasia ya usuluhishi, Mkapa ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania aliteuliwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, jukumu ambalo lilimpatia pia fursa ya kukutana na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres mwezi Februari mwaka 2019 kumpatia hatua zilizofikiwa wakati huo ambapo Burundi ilikuwa inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter