Maskini walipwe kipato cha msingi kila mwezi kuepusha COVID-19- UNDP

Umoja wa Mataifa umesema kuwa kuwapatia watu maskini zaidi duniani kipato cha kujikimu, TBI, kunaweza kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19.
Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP katika ripoti yake iliyochapishwa hii leo, limesema kuwa kipato hicho kitawezesha watu takribani bilioni 3 kusalia nyumbani badala ya kuhaha kwenda kusaka ajira ili kukimu familia.
Ikipatiwa jina Kipato cha msingi cha muda, kulinda watu walio hatarini zaidi katika nchi maskini, ripoti hiyo inakadiria kuwa mpango huo utagharimu dola bilioni 199 kwa mwezi na utalinda watu bilioni 2.7 kote duniani kwenye mataifa 132 yanayoendelea.
Ripoti inatanabaisha kuwa mpango huo unawezekana na unatakiwa haraka wakati huu ambapo janga la Corona linasambaa kwa kasi ya wagonjwa zaidi ya milioni 1.5 kila wiki katika nchi zinazoendelea.
Inachambua takwimu hizo ikisema kuwa katika watu hao, 7 kati ya 10 ni wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ambao hawawezi kupata kipato iwapo watasalia nyumbani wakijikinga dhidi ya Corona.
“Idadi kubwa ya watu hao hawana hifadhi ya jamii kupitia mipango ya bima na wengine ni watu wenye uleavu ambao wameathirika zaidi na janga la COVID-19,” imesema ripoti hiyo.
UNDP imefanya tathmini za athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na COVID-19 katika nchi zaidi ya 60 ambapo ushahidi unaonesha kuwa wafanyakazi ambao hawako katika mifumo ya hifadhi ya jamii hawawezi kubakia nyumbani bila kufanya kazi kujipatia kipato.
“Hii inamaanisha kwamba kipato cha msingi cha muda kinaweza kuwapatia uwezo wa kununua chakula na kulipia gharama za afya na elimu. Na kiwango hiki kinaweza kupatikana kwa sababu malipo ya miezi 6 ya kipato hicho yanahitaji asilimia 12 tu ya gharama zote za kifedha za hatua dhidi ya COVID-19 kwa mwaka 2020,” imesema UNDP.
Shirika hilo linasema kuwa kwa kifupi ni kwamba gharama hizo ni sawa na theluthi moja ya deni la nje la fedha ambazo nchi zinazodaiwa zinapaswa kulipa mwaka huu wa 2020.