IMF yatabiri mdororo wa uchumi duniani kufikia kiwango cha mwaka 2008 lakini kukwamuka mwaka 2021

24 Machi 2020

Shirika la fedha duniani, IMF limesisitiza umuhimu wa hatua za pamoja duniani na mshikamano baina ya nchi zote katika vita dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 huku likisema kuwa mdororo wa uchumi kutokana na janga la sasa utafikia ule wa mwaka 2008 lakini matarajio ya kukwamuka ni mwakani.
 

Mkurugenzi Mwendeshaji wa IMF Kristalina Georgieva amesema hayo alipohutubia kwa njia ya video mkutano wa mawaziri wa fedha na magavana wa Benki Kuu kutoka kundi la mataifa 20, G20.

Amesema kuwa “gharama ya kibinadamu kutokana na COVID-19 tayari haipimiki na kwamba mataifa yanapaswa kushirikiana kulinda watu wake na kudhibiti madhara ya kiuchumi. Huu ni wakati wa mshikamano.”

Mkutano huo ulibeba ujumbe wa mshikamano ambao Bi. Georgieva amesisitiza mambo makuu matatu. Mosi ni “mtazamo wa ukuaji wa uchumi duniani. Kwa mwaka huu wa 2020 ni hasi, mdororo ambao angalau ni mbaya  kama ilivyokuwa wakati wa janga la kifedha duniani au mbaya zaidi. Lakini tunatarajia kukwamuka mwaka 2021. Hata hivyo kufikia hapo ni lazima tupatie kipaumbele udhibiti wa virusi na kuimarisha mifumo ya afya kwingineko. Athari za kiuchumi ni mbaya na zitakuwa mbaya. Lakini kadri virusi vitakavyokoma haraka, vivyo hivyo kukwamuka kiuchumi. Tunaunga mkono kwa dhati hatua za kipekee za kifedha zinazochukuliwa na mataifa mengi ambayo tayari yamechukua hatua kuimarisha mifumo ya afya na kulinda wafanyakazi kazi walioathirika."

Halikadhalika amesema wanakaribisha hatua za Benki Kuu za kulegeza sera za kifedha akisema kuwa hatua hizo ni si kwa maslahi ya nchi husika pekee bali pia kwa uchumi wa dunia nzima na kwamba hata zaidi za aina hiyo zitahitajika.

Mkurugenzi Mwendeshaji huyo wa IFM ametaja hatua ya pili ni kwamba nchi zilizo mbele kiuchumi ziko katika nafasi nzuri za kukabiliana na janga la COVID-19 ilhali nchi zinazoibuka kiuchumi zinakabiliwa na changamoto. “Nchi hizi sasa zimekumbwa na kuondoka kwa mitaji na shughul I za ndani kiuchumi zimedorora kwa kuwa zinakabiliana na janga la Corona. Tangu kuanza kwa corona, wawekezaji tayari wameondoa dola bilioni 83 kutoka kwenye masoko ya nchi zinazoibuka kiuchumi, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa,”  amesema Bi. Georgieva akiongeza kuwa ni kutokana na hali hiyo sasa wanawasiliana na Benki ya Dunia kusaka suluhu ya jambo hilo kwani linawatia hofu kubwa.

Bi. Georgieva ameendelea kutaja jambo la tatu kuwa ni hoja wanayojiuliza ni nini wafanye ili kusaidia wanachama wao ambapo amesema, sasa hivi wanajikita katika ufuatiliaji wa janga hili kuona kuwa hakuna jambo lolote kati ya nchi au la kimataifa linaweza kuwa na madhara. “Tutakusanya fedha za dharura. Takribanimataifa 80 yameomba msaada wetu na tunashirikiana na taasisi nyingine za fedha za kimataifa ili kuwa na suluhu inayoratibika na itakayokuwa na manufaa makubwa,” amesema Mkurugenzi Mwendeshaji huyo wa IMF.

Ameongeza kuwa hivi sasa wanajazia mfuko wa kujenga unafaa kwa majanga ili kusaidia nchi maskini zaidi na wanakaribisa wale ambao tayari wameahidi huku akitoa wito kwa wengine kusaidia. 

Mdororo uchumi wa mwaka 2008 huko Marekani na Ulaya Magharibi ulihusishwa na kile kilichoitwa janga la marejesho ya mikopo ya nyumba ambapo benki zilikopesha fedha wanunuzi wa nyumba ambao hawakuwa na historia nzuri ya kurejesha mikopo na hivyo benki kufikilisika.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter