Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yayumbisha jahazi la vita dhidi ya ukimwi duniani: UNAIDS

Washauri wakisaikolojia  wanazungumza na mama wa mtoto wa miaka tisa katika Kituo cha Tiba ya Antiretroviral Therapy (ART) katika hospitali ya Mumbai, India.
© UNICEF/Hiraj Singh
Washauri wakisaikolojia wanazungumza na mama wa mtoto wa miaka tisa katika Kituo cha Tiba ya Antiretroviral Therapy (ART) katika hospitali ya Mumbai, India.

COVID-19 yayumbisha jahazi la vita dhidi ya ukimwi duniani: UNAIDS

Afya

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya virusi va Ukimwi, VVU  na UKIMWI, UNAIDS imesema vita vya dunia ya kuhakikisha janga hilo lililokatili maisha ya mamilioni ya watu duniani linatokomezwa, ifikapo mwaka 2020 sasa inakwenda mrama.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo ya kuhusu ya hali ya ukimwi duniani, juhudi zinazokwenda kombo ni za kufikia lengo kuu la kutokomeza vitu vitatu katika vita dhidi ya ukimwi ambavyo ni “maambukizi mapya, vifo vinavyohusiana na ukimwi na ubaguzi ifikpo mwaka 2020.”

Akizungumzia kilichochangia hali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima amesema “janga la virusi vya Corona au COVID-19 limeathiri maisha ya watu na uwezo wao wa kumudu kuishi kila mahali, na wakati gonjwa hilo likisambaa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara  ambako kuna kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU, kuna ushahidi kwamba watu wanaoishi wa VVU wako katika hatari kubwa ya kupata COVID-19, magonjwa yanayohusiana na janga hilo na hata kufa.”

Ameongeza kuwa hatua za kupambana na janga hilo kama kufunga kila kitu na watu kusalia majumbani pia zimesababisha wagonjwa kufika kliniki na kupata matibabu ya VVU kuwa shida katika nchi nyingi.

Dawa za kupunguza makali ya VVU , ARV's zimeokoa maisha ya watu wengi duniani kote.
UN
Dawa za kupunguza makali ya VVU , ARV's zimeokoa maisha ya watu wengi duniani kote.

Takwimu za maambukizi

Makadirio ya hivi karibuni ya UNAIDS yanaonyesha kwamba usumbufu wa miezi 6 kwa watu kutoweza kupata dawa za kupunguza makali ya VVU unaweza kusababisha vifo 500,000  zaidi vya magonjwa yanayohusiana na UKIMWI katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara kati ya 2020-2021.

Ripoti hiyo inasema hatari ya VVU miongoni mwa watu wazima iko juu na inatofautiana kwa minajili ya umri, jinsia na kikanda. Kwa mfano Afrika Kusini mwa jangwa la sahara ripoti inasema “wasichana vigori na wanawake wa kati ya umri wa miaka 15-24 ndio walio katika hatari zaidi ya maambukizi mapya ambapo ni mtu 1 kati ya 4."

Kwa kikanda bado Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kunashikilia nafasi ya juu  huku ripoti ikitaja maeneo yalitoathirika zaidi kuwa ni Mashariki na Kusini mwa bara hilo ambako vigori na wasicha ni asilimia 30 ya maambukizi yote mpaya ya HIV duniani.

Nje ya Afrika kwa mujibu wa ripoti mwaka 2019 maambukizi mengi mapya yalikuwa miongoni mwa wanaumme yakiongozwa na asilimia 79 Ulaya Mashariki na Kati na Amerika Kaskazini huku visiwa vya Caribbea vikishikilia asilimia 57.

Duniani kote mwaka 2019 karibu robo ya maambukizi mapya, sawa na asilimia 23 ya maambukizi,  yalikuwa ni miongoni mwa wanaumme mashoga na kundi hilo ndio limeongeza kwa maambukizi mapya pia Asia na Pasifiki, Amerika ya Kusini na karibu asilimia 64 Ulaya Mashariki na Kati na Amerika Kaskazini.

Ripoti pia imetaja kwamba maambukizi yatokanayo na kujidunga madawa ya kulevya kote duniani yalikuwa karibu asilimia 10 ya maambukizi yote mapya. 

Na kwa Ulaya Mashariki,  Kati na Asia yalikuwa asilimia 48 huku nafasi ya pili ikienda Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kwa asilimia 43.

Mafanikio yaliyopatikana

Mbali ya changamoto ripoti  imekuwa na Habari njema pia kwamba ongezeko la dawa za kupunguza makali ya VVU limesaidia kuokoa vifo milioni 12.1 vinavyohusiana na ukimwi tangu mwaka 2010.

“Na vifo 690,000 vilisababishwa na ukimwi mwaka 2019 duniani kote  na hiyo ilikuwa ni idadi ndogo zaidi ya vifo vya ukimwi kurekodiwa tangu mwaka 1993 na ni punguzo la asilimia 39 la vifo tangu mwaka 2010." kwa mujibu wa ripoti.

UNAIDS inakadiria kwamba watu milioni 24.4 walipata fursa ya dawa za kupunguza makali ya VVU mwaka 2019 na kwamba kulikuwa na watu milioni 38 duniani kote waliokuwa wanaishi na VVV  mwaka huo.

Lakini pia ripoti imeweka bayana kwamba mwaka huo wa 2019 watu milioni 1.7 wapya waliambukizwa VVU ikiwa ni idadi ndogo zaidi ya maambukizi mapya kwa mwaka tangu 1989, lakini wakati huohuo watu 690,000 walifariki dunia kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukimwi 2019.

Kwa ujumla ripoti hiyo inasema watu milioni 75.7 wameambukizwa VVU tangu kuanza kwa ugonjwa huo katika miaka ya 1980 na watu milioni 32.7 wamepoteza maisha duniani kote.