Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 hatarini kuongeza idadi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI- UNAIDS

Lighton,  mtoto wa umri wa mwaka mmoja akipokea dawa za kupunguza makali ya ukimwi nyumbani kila siku katika eneo la Mbarara Uganda.
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Lighton, mtoto wa umri wa mwaka mmoja akipokea dawa za kupunguza makali ya ukimwi nyumbani kila siku katika eneo la Mbarara Uganda.

COVID-19 hatarini kuongeza idadi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI- UNAIDS

Afya

Umoja wa Mataifa umetaka serikali duniani kupitisha malengo mapya ya kukabiliana na Virusi Vya Ukimwi, VVU na UKIMWI ili kuepusha mamia ya maelfu ya maambukizi na vifo vinavyohusiana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona au COVID-19.
 

Chombo hicho kimesema hayo kupitia ripoti mpya ya shirika lake la kupambana na UKIMWI, UNAIDS, kikionya kuwa janga la Corona limepeleka mrama harakati za kukabili UKIMWI na kwamba malengo ya 2020 hayajafikiwa.

Ripoti hiyo mpya ikipatiwa jina, kuhimili majanga kwa kujali kwanza watu imetolea kuelekea siku ya UKIMWI duniani tarehe Mosi mwezi Desemba.

UNAIDS inataka nchi zijifunze kutokana na hasara ya kutowekeza vya kutosha katika mifumo ya afya na ziongeze hatua za kumaliza UKIMWI na dharura nyingine za kiafya duniani.

Gharama ya kibinadamu

Ikitaja takwimu mpya zinazoonesha athari hasi za muda mrefu za COVID-19 kwenye harakati za kutokomeza UKIMWI, UNAIDS inasema kunaweza kukawepo na maambukizi mapya takribani 300,000 kati ya sasa na mwaka 2022 na hadi vifo 148,000 vihusianavyo na UKIMWI.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima amesema kushindwa kwa pamoja kuwekeza vya kutosha katika hatua za kina, zinazojali utu na haki za kila mtu kumesababisha gharama kubwa.

Amesema kutekeleza peke yake miradi inayokubalika kisiasa hakutabadli mwelekeo wa maambukizi ya COVID-19 au hata kutokomeza AIDS.

Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI-ARV
Photo: Sean Kimmons/IRIN
Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI-ARV

Bi. Byanyima amesema “ili kurejesha hatua za kimataifa kwenye mwelekeo sahihi, kunahitajika kuwaweka watu mbele na kushughulikia ukosefu wa usawa unaochochea janga hilo kuendelea.”

Ripoti inasema ijapokuwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Botswana na Eswatini zimefikia au hata kuvuka malengo ya mwaka 2020, bado nchi nyingi ziko nyuma.

Turejee kwenye mwelekeo sahihi wa kukabili UKIMWI

Nyaraka hiyo ya UNAIDS ina mapendekezo kadhaa kwa malengo ya 2025 ambayo yanazingatia hatua zilizochukuliwa na mataifa yaliyofanikiwa zaidi kukabiliana na UKIMWI.

Malengo yanajikita zaidi katika kupanua wigo wa huduma za VVU na afya ya uzazi pamoja na kuondoa sheria za kibaguzi, kinyanyapaa na zinazoharamisha baadhi ya mambo.

Lazima kujali watu mathalani vijana wa kike, wasicana, barubaru, makahaba na mashoga.
UNAIDS inasema iwapo malengo hayo yanafikiwa, dunia itakuwa imerejea kwenye mwelekeo wake wa kutokomeza UKIMWI kama kitisho cha afya ya umma ifikapo mwaka 2030.