Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wenye UKIMWI hatarini maradufu kufa kwa Corona

Wazazi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, vvu wakiwa katika kliniki yao ya kuwapatia usaidizi wilayani Kamuli nchini Uganda.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Wazazi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, vvu wakiwa katika kliniki yao ya kuwapatia usaidizi wilayani Kamuli nchini Uganda.

Wenye UKIMWI hatarini maradufu kufa kwa Corona

Afya

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI inaonesha kuwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi au VVU wako katika hatari zaidi ya kuugua ugonjwa wa Corona au COVID-19 na hata kufariki dunia lakini bado wananyimwa haki ya kupata chanjo dhidi ya Corona.

Ikitolewa leo huko Geneva, Uswisi na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS, ripoti inaitwa Kukabiliana na Ukosefu wa Usawa mwaka 2021 na ina ushahidi dhahiri kuwa ukosefu wa usawa unazuia watu hao wanaoishi na VVU washindwe kupata chanjo dhidi ya COVID-19 na huduma za VVU.

Tafiti zilizofanyika Uingereza na Afrika Kusini zimeonesha kuwa hatari ya mtu anayeishi na VVU kufariki dunia kwa COVID-19 ni maradufu zaidi ya mtu asiye na VVU.

Hali ikoje barani Afrika

Katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara ambako kuna asilimia 67 ya watu wote wanaoishi na VVU duniani kote, ni chini ya asilimia 3 ya watu hao ndio wamepata angalau dozi ya kwanza ya COVID-19 hadi mwezi huu wa Julai.

Wakati huo huo, huduma za kinga dhidi ya VVU pamoja na matibabu zinaengua makundi muhimu na watoto na barubaru.

Makundi yaliyo hatarini yana nafasi kubwa zaidi ya kuathiriwa na majanga kama vile COVID-19 na UKIMWI
UNAIDS/Daniel Msirikale
Makundi yaliyo hatarini yana nafasi kubwa zaidi ya kuathiriwa na majanga kama vile COVID-19 na UKIMWI

Ripoti hiyo inasema chanjo dhidi ya COVID-19 zinaweza kuokoa maisha ya mamilion iya watu katika nchi zinazoendelea, “lakini zinahodhiwa nan chi tajiri na mashirika katika uzalishaji na usambazaji kwa lengo la kujipatia faida. Hii ina madhara makubwa katika mfumo wa afya kwenye nchi zinazoendelea kwani mifumo hiyo imezidiwa uwezo. Mfano Uganda, ambako viwanja vya mpira wa miguu vimegeuzwa kuwa hospitali za muda.”

Akizungumzia hali hiyo ya utata na sintofahamu kuhusu pengo la utoaji chanjo kati ya nchi tajiri na zile maskini, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima amesema, “nchi tajiri barani Ulaya zinajiandaa kufurahia majira ya kiangazi kwa kuwa wananchi wao wamepata chanjo dhidi ya COVID-19 ilhali nchi maskini ziko katika janga”
Bi. Byanyima amesema dunia imeshindwa kupata somo kutokana na VVU wakati mamilioni ya watu walioponyima dawa muhimu za kuokoa maisha yao, walikufa kwa sababu ya ukosefu wa usawa. “Hii haikubaliki.”

Vikwazo vya COVID-19 vilififisha huduma za VVU

Vikwazo vya kudhibiti ugonjwa wa Corona vilivuruga upimaji wa VVU katika nchi nyingi  na kusababisha kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa uchunguzi, kuelekeza watu kwenda vituo kupata huduma za VVU na hata kuanza kwa matibabu.
Mathalani huko KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini, kulikuwa na anguko la asilimia 48 la upimaji VVU baada ya serikali kutangaza hatua za kuzuia watu kutembea kudhibiti COVID-19 mwezi Aprili mwaka 2020.

Utoaji wa huduma za VVU ulipungua kwa sababu wahudumu 28,000 wa VVU katika jamii walielekezwa katika kupima watu COVID-19.

Vipimo vya virusi vya ukimwi.
Public Health Alliance/Ukraine
Vipimo vya virusi vya ukimwi.

Asilimia 65 ya maambukizi mapya milioni 1.5 ya VVU kwa mwaka 2020 yalikuwa miongoni mwa makundi muhimu kama vile wanaojidunga dawa za kulevya, wanawake waliobadili jinsia, makahaba, mashoga na wasagaji.

Makundi hayo bado yananyanyapaliwa katika kupata huduma za VVU katika nchi nyingi.

Ukosefu wa usawa katika huduma si jambo linalotokea hivi hivi bali ni matokeo ya sera na hatua mahsusi za kuengua badala ya kujumuisha, amesema Bi.Byanyima.

Jawabu la kushinda janga lolote ni kuhakikisha kuna usawa

Mathalani makundi hayo muhimu yanaenguliwa na kuonekana ni wahalifu kwa kujitambulisha kwa jinsia zao wanazotaka.
“Ni miaka 40 tangu kuanza mapambano dhidi ya VVU. Mafanikio na anguko vimetufundisha kuwa hatuwezi kujiandaa kwa janga au kushinda janga lingine iwapo hatutasambaratisha ukosefu wa usawa na kusongesha hatua zinazojali watu, haki na kila jamii,” amesema Bi. Byanyima.