Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yachukua hatua za ziada kudhibiti kusambaa kwa COVID-19 kambi ya wakimbizi Dadaab

wakimbizi wa Kisomali katika kambi ya Daadab, Kenya.
UN Photo.
wakimbizi wa Kisomali katika kambi ya Daadab, Kenya.

UNHCR yachukua hatua za ziada kudhibiti kusambaa kwa COVID-19 kambi ya wakimbizi Dadaab

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR linasambaza chakula na bidhaa za kujisafi kwa wakimbizi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya ikiwa ni hatua ya kuudhibiti ugonjwa wa COVID-19.

Wakimbizi wamejipanga katika mstari ili kupokea chakula, lakini kwa tahadhari ya kujikinga na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19, wamezingatia umbali kati ya mtu na mtu.

UNHCR, kwa pamoja na shirika la mpango wa chakula duniani WFP kwa kushirikiana nan a wadau wengine, wanatoa mgao wa chakula mara mbili katika kambi ya wakimbizi ya Dadaabnchini Kenya. Pia wanasambaza bidhaa za kujisafi kama vile sabuni, vifaa kama madumu au jerikeni ili kupunguza uhitaji wa kuwa na misongamano mikubwa na misururu lengo likiwa ni kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona kambini. 

Maafisa wa UNHCR wanasaidia kuwaelekeza waliofika kupokea chakula. Vituo vya kunawa mikono vimewekwa katika meaneo ya kusambazia chakula, katika shule na masoko. Vituo vya afya vimewezeshwa kwa kuwekewa maeneo ya kutenga watu kwa muda maalumu wakati wa uangalizi.

Kama ilivyokuwa kwa upande wa wanawake, upande wa wanaume nako wamepanga mistari iliyozingatia umbali kati ya mt una mtu, na pia kuna afisa wa UNHCR anayewaelekeza wakati wa kwenda na mahali pa kwenda lakini kabla yah apo wanafanya usafi wa mikono kwa maji tiririka kutoka katika matenki yaliyosambazwa katika eneo hilo.

Tahadhari zote zinachukuliwa ikiwemo kupima joto, maelekezo ya kuelimisha watu kuhusu COVID-19 yaliyobandikwa ukutani, kuepuka kugusana na hata uvaaji wa barakoa.

Kufikia mwezi Mei mwaka huu wa 2020 makazi ya kambi ya Dadaab yako kaskazini mwa Kenya, yanaripotiwa kuhifadhi  wakimbizi na wasaka hifadhi 200,000, ambayo ni idadi kubwa inayoweza kuwa hatarini ikiwa hatua kama hizi zinazofanyika zisipozingatiwa.