Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake Dadaab Kenya wajumuika kukabili misimamo mikali

Wanawake katika kambi ya Dadaab nchini Kenya
UN Women
Wanawake katika kambi ya Dadaab nchini Kenya

Wanawake Dadaab Kenya wajumuika kukabili misimamo mikali

Wanawake

Nchini Kenya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women kwa ushirikiano na wadau wanajengea uwezo wajenzi wa amani mashinani hata kwenye maeneo yenye changamoto kama vile kambi ya wakimbizi ya Daadab kwenye kaunti ya Garissa nchini humo kwa lengo la kuepusha vijana kutumbukizwa kwenye vikundi vyenye msimamo mkali.

UN Women inafanya hivyo kupitia warsha inazoendesha kwa ushirikiano na mashirika ya kiraia ya wanawake kama vile WomanKind Kenya ambapo katika moja ya warsha huko kambini Daadab, Nimo Dubat, mwenyekiti wa chama cha wanawake wachuuzi sokoni anaelezea umuhimu wa warsha hizo. Nimo Dubat anasema “Kwa upande wa usalama, wanawake na vijana ndio wanaweza kufuatilia, sisi ndio vijana tumezaa na tunajua ambaye anaanza kuleta shida nyingi. Katika watoto wetu, mama ndiye mzazi, mama ndiye anajua ambaye anaanza tabia mbaya. Mama ndiye anajua nani ameingia kwenye mtaa mgeni, na nani Jirani yake amepokea mgeni, hata tumetengeneza kikundi cha wanawake wa nyumba 10. Hata kuna wasichana wajumbe wa nyumba 10. Sasa tunataka tupatiwe nguvu, tushikamane na polisi kwenye ulinzi. Mama ndiye anabeba mzigo wa shida yote.

Nasiba Abdi Farah mkazi wa Daadab na mnufaika wa warsha hiyo iliyojumuisha wanaume na vijana wa kike na wa kiume, hakuficha hisia zake akisema kupitia mafunzo waliyopata. Nasiba Abdi Farah anasema "Yule kijana ambaye sitamuona nitauliza kwa wenzake ameenda wapi? Ameenda mpakani? Basi nitaenda kwa mama na kumuuliza mtoto wake ameenda kufanya nini mpakani? Akisema sijamuona? Namueleza tafuta kijana wako na umlete.”

Warsha hii ilipatia fursa pia viongozi wa eneo la Daadab kushirkiana na mashirika yenye mtazamo sawa kupitisha na kuridhia na kuanza kutekeleza Mpango wa Utekelezaji wa Kaunti ya Garissa wa kuzuia na kukabiliana na misimamo mikali.