Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nitarejea Kakuma na Dadaab kuwasaidia wakimbizi wenzangu - Nhial Deng 

Nhial Deng, wakati wa mahojiano na Flora Nducha wa UN News Kiswahili katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Nhial Deng mwenye asili ya Sudan Kusini amekuwa mkimbizi tangu alipozaliwa mwaka 1999 nchini Ethiopia. Sasa anasomea shahada y
UN/Anold Kayanda
Nhial Deng, wakati wa mahojiano na Flora Nducha wa UN News Kiswahili katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Nhial Deng mwenye asili ya Sudan Kusini amekuwa mkimbizi tangu alipozaliwa mwaka 1999 nchini Ethiopia. Sasa anasomea shahada yake ya kwanza katika masuala ya kimataifa na mawasiliano nchini Canada.

Nitarejea Kakuma na Dadaab kuwasaidia wakimbizi wenzangu - Nhial Deng 

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu ukiwa umehitimishwa kwa mwaka huu wa 2022, mmoja wa vijana waliohudhuria ni Nhial Deng ambaye anauishi msemo wa wahenga wa usitupe mbachao kwa msala upitao.

Nhial Deng ni mkimbizi ambaye angalau sasa anaanza kuuona mwanga katika maisha yake nchini Canada lakini moyo wake bado unaendelea kuwakumbuka wenzake aliowaacha kambini Kakuma na Daadab nchini Kenya.  

Historia yake ya ukimbizi ilianza pindi ambapo baba yake aliikimbia vita Sudan Kusini hadi Ethiopia ambako baadaye Nhial Deng alizaliwa mwaka 1998. Nako huko Ethiopia mwaka 2010 kukaibuka machafuko, mtoto Nhial Deng akakimbilia Kambini Kakuma, Kenya ambako aliishi kwa miaka 11 hadi alipofanikiwa kwenda masomoni Canada. Katika mazungumzo haya na Flora Nducha, Nhial Deng anaanza kwa kueleza alivyopata fursa kuondoka katika kambi ya wakimbizi na mipango yake ya kuwasaidia wengine hasa katika elimu.   

Anasema alipokuwa katika kambi ya Kakuma alikuwa kiongozi wa vijana akishirikishwa katika shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wengine ikiwemo serikali ya Kenya.  

“Nilikuwa ninashughulikia masuala ya wakimbizi kambini Kakuma na nilikuwa ninakaa kwenye Kamati ninaongea kuhusu matatizo waliyokuwa wanayapitia wakimbizi waliokuwa wanaishi Kakuma. Nilifanya hivyo nilipokuwa ninasoma na nilipomaliza shule mwaka 2018 nilianzisha kampuni kusaidia wakimbizi walioko Kakuma.” Anaeleza Nhial Deng. 

Nhial anaeleza kuwa walifanya shughuli za kuhamasisha amani, michezo ili watu waje wacheze pamoja wawe na furaha kwa kuwa kulikuwa na shida nyingi ambazo walikuwa wanapitia wakati huo. Shughuli hiyo aliiifanya kwa miaka miwili hadi mwaka 2020 ambapo alianza kutafuta fursa za kwenda kupata elimu ya juu na akapata Chuo nchini Canada, ambao walimpatia ufadhili wa kusoma ngazi ya chuo kikuu ambako sasa ameanza kusoma masuala ya kimataifa na mawasiliano.  

Changamoto za elimu zinazowakabili wakimbizi 

Nhial Deng anasema kuna changamoto nyingi zinazowakabili wakimbizi katika harakati zao za kusaka elimu au kuendelea na elimu baada ya kuzikimbia nchi zao.  

“Moja ni za makaratasi (nyaraka mbali), wakimbizi wakikimbia nchi zao wengi wanaenda kwenye kambi za wakimbizi huwa hawana fursa ya kutafuta karatasi zao kama Hati za kusafiria, vyeti vya shule na wengine wanakuja bila nyaraka zozote na wakifika nchi mwenyeji wao inakuwa vigumu kwenda shule kwa kuwa wanaulizwa nyaraka zenu za shule ziko wapi. Hawana.” Anaeleza Deng akiongeza changamoto nyingine kuwa ni lugha, “nchi nyingi ambazo wakimbizi wanatoka hawaongei kwa mfano lugha kama Kiswahili, Kingereza, Kifaransa na hivyo wakienda katika nchi fulani inakuwa vigumu waende shule kwa kuwa hawasilkii lugha ambayo inatumika kufundishia shuleni.” 

Kama alivyosema kijana huyu changamoto zinazowakabili wakimbizi katika suala la elimu ni nyingi akiongeza kuwa wakimbizi wengi wakifika katika nchi nyingine wanakuwa hawana pesa za kulipa ada ya shule na hivyo wanashindwa kuendelea na masomo. “Njia pekee inakuwa ni wakipata ufadhili ndipo wanasoma.” 

Ni marekebisho gani katika elimu yafanyike ili kusaidia wakimbizi popote walipo? 

Nhial anashauri kwamba ni mhumi wakimbizi wanapofika katika nchi fulani wajumuishwe katika mfumo wa elimu wa nchi hiyo ili wasipoteze fursa ya kwenda shule.  

Nyingine anazisihi nchi wahisani wasaidie nchi ambazo zinawapokea wakimbizi, “ndio wawe na raslimali za kutosha kusaidia wakimbizi.” 

Na mwisho ushauri wake ni kuhakikisha kunawa na amani kwani wakimbizi wengi wanatamani kurejea makwao iuli waendelee kusoma na “kuishi maisha yao kwa amani na furaha.” 

Nhial Deng, wakati wa mahojiano na UN News Kiswahili katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Nhial Deng mwenye asili ya Sudan Kusini amekuwa mkimbizi tangu alipozaliwa mwaka 1999 nchini Ethiopia. Sasa anasomea shahada yake ya kwanza ka
UN/Anold Kayanda
Nhial Deng, wakati wa mahojiano na UN News Kiswahili katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Nhial Deng mwenye asili ya Sudan Kusini amekuwa mkimbizi tangu alipozaliwa mwaka 1999 nchini Ethiopia. Sasa anasomea shahada yake ya kwanza katika masuala ya kimataifa na mawasiliano nchini Canada.

Sitatupa mbachao kwa msala upitao 

Kijana Nhial Deng anasema pamoja na kwamba amepata fursa ya kuishi na kusoma nchini Canada, akihitimu masomo yake atarejea ‘nyumbani’ kuwasaidia wakimbizi wenzake aliowaacha katika kambi za Kakuma na Dadaab.  

“Niongee nao waendelee kusoma wasikate tamaa kwenye maisha na pia ningependa kufanya kazi na Canada siku moja, ili nihakikishe wanapoongea katika Umoja wa Mataifa wahakikishe wahakikishe wanasaidia wakimbizi.” Anasisitiza Nhial.