Serikali lazima ziwalinde wahamiaji wakati wa COVID-19

26 Mei 2020

Wataalam wa haki za binadamu leo wametoa wito kwa serikali kulinda haki za wahamiaji na familia zao bila kujali hadhi zao za uhamiaji wakati na baada ya janga la virusi vya corona au COVID-19.

Wataalam hao Can Ünver ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu wafanyakazi wahamiaji na Felipe González Morales mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wahamiaji wamesema “Haki za wafanyakazi wahamiaji kimataifa hususan walio katika sekta muhimu lazima zihakikishwe na na hatua kuchukuliwa kulinda afya zao. Maelfu ya wahamiaji hivi sasa wamekwamba katika mipaka kote duniani, barani Asia, Afrika, nchi za Amerika au baharini kwenye fukwe za Ulaya.”

 Mwongozo mpya kuhusu uhamiaji

Wataalam hao wameyasema hayo wakati wakitangaza chapisho mtandaoni la muongozo muhimu kuhusu athari za janga la COVID-19 kwa haki za binadamu za wahamiaji.

Katika muongozo huo wenye vipengele 17 kwa serikali wataalam wamezitaka serikali kuhakikisha haki na muendelea wa kanuni kwa ajili ya watu wanaohitaji ulinzi wa kimataifa , ikiwemo fursa ya mipaka yao na kuwataka kuendelea na operesheni za kuwasaka na kuwaokoa watu waliopatwa na dhoruba baharini.

Wamesisitiza kwamba “serikali zinapaswa kuhakikisha fursa ya huduma za kijamii kwa wahamiaji na familia zao ambapo katika baadhi yan chi wameonekana kuwa na idadi kubwa ya maambukizi na vifo kutokana na COVID-19. Wahamiaji ambao hawako katika hali ya kawaida au hawana nyaraka wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi. Wanafaka kazi zisio na uhakika mara nyingi bila mafao au haki za malipo ya bukosa ajira na katika baadhi ya matukio wamekuwa wakiachwa na hatua za nchi za msaada wa kijamii, licha ya mchango mkubwa wa kiuchumi wanaoutoa katika jamii kama wahamiaji.Kwa muktada huu tunatoa wito kwa serikali kuchagiza uhalalishaji wa wahamiaji walio katika hadhi zisizo rasmi.”

UNICEF/Ashley Gilbertson VII
Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani

 

Chonde chonde wajumuisheni wahamiaji

Kamati ya Umoja wa Mataifa na wataalam maalum wametoa wito kwa serikali kote duniani “kujumuisha wafanyakazi wahamiaji katika mipango na sera za kitaifa za kuzuia na kupambana na COVID-19, ambazo zinazingatia jinsia, umri na watu tofauti na kuheshimu haki zao za afya.”

Katika mwongozo huo wataalam pia wametizaka nchi kujumuisha wahamiaji na familia zao katika sera za kujikwamua kiuchumi wakichukulia umuhimu wa haja ya kujikwamua na utumaji wa fedha nyumbani.

 “Tunataka kuitonya dunia kwamba athari za COVID-19 katika uwezo wa wahamiaji kufanyakazi umeshasababisha kuchuka kwa kiwango cha kimataifa cha utumaji fedha kwa familia zao katika nchi walikotoka, ambazo kuishi kwa familia hizo kunategemea fedha hizo zinazotumwa, lakini pia katika nchi ambako ndio chanzo cha fedha zinazotumwa kwa uchumi wao. Familia hizo sasa zinahaha kuishi.”

Wamesisitiza kwamba serikali zinapaswa kutekeleza mikakati ili kutathimini matumizi ya vituo vya kushikilia wahamiaji kwa mtazamo wa kupunguza idadi yao mahabusi na kufikia kiwango cha chini iwezekanavyo. Na kuziachalia mara moja familia zenye Watoto na Watoto wasio na wazazi ama walezi kutoka kwenye mahabausu hizo za wahamiaji na kuwapeleka kwenye vituo maalum vya kijamii kama njia mbadala huku wakipewa haki zote na huduma.

Na mwisho wataalam hao wamesema “serikali lazima zifikirie kusitsha kwa muda kuwarejesha kwa nguvu au kuwafukuza wahamiaji hao wakati huu wa janga la corona” wakiongeza kwamba idadi kubwa ya wahamiaji wamerejeshwa kwa lazima au kufukuzwa katika nchi mbalimbali wakibeba ugonjwa huo wa COVID-19.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter