Mashirikisho na jumuiya 200 yaonesha mshikamano na waathirika wa COVID-19 wanaobaguliwa

1 Julai 2020

Viongozi wa jumuiya za ughaibuni na mashirika ya kijamii kutoka kote duniani wamekuja pamoja kutuma ujumbe ulio bayana  na wa mshikamano na watu wanaokabiliwa na vitendo vya chuki dhidi ya wageni, ubaguzi na hata ukatili kutokana na janga la corona au COVID-19 kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

Jumuiya 200 zinazosaidia jamii zilizoko ughaibuni katika nchi zaidi ya 150 zimetia saini taarifa ya pamoja ambayo lengo lake ni kuanzisha “kawaida mpya” ambayo jamii zitaweza kubaini uwezo walionayo katika utofauti wao na kuweza kusaidiana.

Taarifa hiyo ambayo imeandaliwa na IOM kupitia jukwaa lake la kimataifa la ughaibuni, Diaspora imetiwa msukumo mkubwa na shirikisho la wanataaluma wa Kichina nchini Uingereza, Jukwaa la maendeleo ughaibuni la Afrika na Ulaya, mtandao wa Afrika ughaibuni (AND) na muungano kwa ajili ya Venezuela. (Coalición por Venezuela.).

Akizungumzia taarifa hiyo ya pamoja mkurugenzi mkuu wa IOM Antonio Vitorino amesema, “inasisitiza umuhimu wa haki ya kijamii, kupinga ubaguzi wa rangi na haja ya umoja miongoni mwa watu bila kujali utaifa, rangi ya ngozi yao na utamaduni wa walikotoka hasa katika wakati huu wa changamoto kubwa na katika wakati wa kujikwamua na janga hili la COVID-19."

Bwana Vitonio ameongeza kuwa “sasa kuliko wakati mwingine wowote usalama wa jamii yetu kwa ujumla unategemea ulinzi kwa walio hatarini zaidi. Chuki kwa wageni na ubaguzi wa rangi vinadidimiza hatua zetu za kupambana na COVID-19 na juhudi za kushughulikia changamoto za kiuchumi na kijamii ambazo ni mzigo mkubwa kwa wasiojiweza na wanaotengwa katika jamii zetu wakiwemo wahamiaji.”

Ili kugeuza maneno ya taarifa hiyo kuwa vitendo IOM inasema  waliotia saini watakutana tena tarehe 8 Julai kuunda muungano wa kimataifa kwa ajili ya walio ughaibuni na kuahidi kufanyakazi pamoja kushughulikia changamoto zinazojitokeza kutokana na hali ya sasa.

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter