Hakuna uhalali wowote wa kuwashambulia raia Afghanstan-UNAMA

13 Mei 2019

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa nchini Afghanistan, ameeleza kusikitishwa kwake na ongezeko la vurugu katika maeneo mbalimbalimbali ya nchi wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.

Mwakilishi huyo Tadamichi Yamamoto ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA amesema hayo leo kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Kabul, nchini Afhganistan.

Amelaumu  wanamgambo wa Taliban kwa matukio ambayo kwa makusudi yanawalenga wananchi kama lile la tarehe 8 mwezi huu wa Mei mjini Kabul dhidi ya shirika lisilo la kiserikali ambapo wananchi wanane waliuawa na wengine 28 walijeruhiwa.

Bwana Yamamoto amesema, “hakuwezi kuwa na uhalalishaji wa aina yoyote wa mashambulizi ya makusudi dhidi ya wananchi. Waathirika wakubwa walikuwa waafghanstan. Ni dhahiri sana kwamba tendo la awali la vurugu lilifanyika dhidi ya shirika la maendeleo ambalo raia walikuwa wakijitahidi kuboresha maisha ya wananchi wote.”

Tukio lingine ni shambulizi la kujitolea kufa lililotekelezwa na wataliban dhidi ya Makao Makuu ya Polisi nchini Afghanstan katika eneo la Pul-e-Khumri, jimbo la Baghlan, raia wengi walijeruhiwa, miongoni mwao wakiwemo wanawake na watoto.

Halikadhalika amesema wanachunguza kwa kina madai ya kwamba raia walijeruhiwa kutokana na shughuli za anga za jeshi la washirika kwenye majimbo ya Farah na Nimroz dhidi ya viwanda vya utengenezaji wa madawa ya kulevya. 

Maeneo hayo hayafikiki kirahisi na kuna changamoto nyingi za uendeshaji ili kuweza kuthibitisha hali za watu wanaodaiwa wameathiriwa na shughuli hizi za kijeshi.

Amerejelea wito kwa pande zote kusitisha mapigano wakati huu wa mfungo wav mwezi mtukufu wa Ramadhan na watekeleze wajibu wao wa kuwalinda wananchi. 

Bwana Yamamoto ametumia pia taarifa  yake kutuma salamu za ramibrambi kwa familia za waathirika na kuwatakia kupona haraka wale wote walioathirika na vurugu za hivi karibuni.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud