Sherehe za Eid zaleta ahueni kwa wananchi wa Afghanistan
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA umekaribisha tangazo la serikali nchini humo la kusitisha mapigano bila masharti yoyote kwa ajili ya sherehe za Eid El Haj, na hivyo umetoa wito kwa pande kinzani kwenye mzozo kutumia fursa hiyo kukomesha ghasia.
Taarifa ya UNAMA iliyotolewa leo mjini Kabul, imemnukuu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Tadamichi Yamamoto akisema kuwa sitisho la mapigano ambalo limekubaliwa na pande zote litaleta matumaini ya kufanyika kwa mazungumzo kati ya makundi husika ili kupata suluhu ya kisiasa.
Ameongeza kuwa “ni muhimu kuchukua nafasi hii kuzungumzia hatua za kumaliza mgogoro ili raia wote wa Afghanistan waweze kufurahia amani wanayotaka.”
Miezi iliyotangulia usitishwaji wa mapigano umeokoa maisha mengi ya raia na hivyo kudhihirisha jinsi raia wa Afghanistan wanataka mgogoro huo uishe.
Katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu, raia 1,692 waliuawa katika mapigano kati ya serikali na wapiganaji wa Taliban, ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika muongo mmoja.
Mwaka huu pekee zaidi ya shule 130 nchini Afghanistan zilishambuliwa na vituo viwili vya afya viliharibiwa kabisa.
Habari zinasema kama hiyo haitoshi, matukio ya kushambulia watoa huduma za misaada nayo yaliongezeka kwa asilimia 20, ambapo wafanyakazi 23 waliuawa, 37 walijeruhiwa na 74 walitekwa nyara