Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yapokea zaidi ya dola milioni 4 kusaidia nchi kupambana na COVID-19

Miongoni mwa vifaa vya kusaidia kupima COVID-19 ambavyo Morocco imepokea kutoka IAEA.
AFRA/IAEA
Miongoni mwa vifaa vya kusaidia kupima COVID-19 ambavyo Morocco imepokea kutoka IAEA.

IAEA yapokea zaidi ya dola milioni 4 kusaidia nchi kupambana na COVID-19

Afya

Mpango wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA wa kusaidia kutokomeza ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, umepata msukumo mpya baada ya kampuni ya kijapani ya kutengeneza dawa, TAKEDA kuchangia zaidi ya dola milioni 4.7.
 

Fedha hizo kutoka kampuni hiyo ambayo ni moja ya kampuni kubwa za kutengeneza dawa duniani, utawezesha IAEA, kuongeza msaada wake wa dharura kwa nchi wanachama ambazo zinahitaji mbinu za haraka na za kisasa za kudhibiti virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000,000 duniani kote.

Mapema mwezi Machi mwaka huu, IAEA ilitangaza kupatia nchi zitakazoomba msaada, mashine salama za kuchunguza virusi vya Corona sambamba na ushauri wa kitaalamu na muongozo wa kiufundi.

Hadi sasa mataifa 119 yameshawasilisha maombi yao IAEA yakitaka kutumia teknolojia ya nyuklia ambayo ni ya uhakika zaidi katika kutoa majibu ndani ya saa chache.

Mataifa 16 kati ya hayo tayari yamepokea mashine, vifaa vya kujikinga, na vifaa vya maabara na mataifa mengine yatapokea misaada ya aina hiyo siku na wiki chache zijazo.

Nchi ambazo zimeshapokea msaada huo ni pamoja na  Morocco,Bosnia na  Herzegovina, Burkina Faso, Iran, Latvia, Lebanon, Malaysia, Nigeria, Peru, Senegal, Thailand na Togo.

Akizungumzia mchango wa TAKEDA, ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kutolewa na kampuni hiyo kwa wakati mmoja, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi amesema, “mchango wa TAKEDA uwezesha IAEA kuongeza kasi ya kusaidia dunia kukabili janga la Corona na kupeleka vifaa vingi zaidi vya uchunguzi kwa nchi ambazo zinahitaji.”

Amesema mchango huo unaongezea kwenye bajeti ya ziada ya dola zaidi ya milioni 23 ambazo tayari nchi 23 wanachama wa shirika hilo wameshaahidi kwa ajili ya kusaidia IAEA kukabili COVID-19.

Mradi huu wa sasa, ni mradi mkubwa zaidi wa ushirikiano wa IAEA kwa kiwango cha fedha na idadi ya wanufaika tangu shirika hilo lianzishwe mwaka 1956.
Bwana Grossi amesisitiza kuwa ana imani kuwa wataweza kukabili janga la Corona kwa pamoja.