Janga la COVID-19 ni kengele ya kutuamsha sote:Guterres

18 Mei 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema janga la virusi vya corona ni kengele ya kutuamsha sote hivyo ni wakati wa kushikamana na kusaka kinga na tiba ya kuutokomeza ugonjwa huu unaoiyumbisha dunia. 

Antonio Guterres ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa Baraza la afya Duniani linalofanyika kwa njia ya mtandao Geneva Uswisi akiongeza kuwa “janga hili limedhihirisha udhaifu wa dunia, licha ya utaalam wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia yaliyopatikana katika miongo ya karibuni virusi hivi vimetuadabisha. Hadi sasa hatujui jinsi gani ya kuvitokomeza, kuvitibu au chanjo ya kujikinga navyo na hatujui lini tunaweza kufanya haya.”

Katibu mkuu amesisitiza kwamba hata hivyo udhaifu ulioanikwa na COVID-19 sio tu kwamba umeathiri mifumo ya afya bali kila nyanja ya maisha, duniani kote na taasisi zote.

Ameliambia Baraza hilo la Afya kwamba udhaifu wa kuratibu juhudi za kimataifa kupambana na janga hili umewekwa wazi kama dunia ilivyoshindwa katika juhudi zingine za kimataifa ikiwemo vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, kudhibiti uzalishaji wa nyuklia, kukomesha uhalifu wa mtandaoni kwani vita vya mtandao tayari vimeshaanza na kutozingata sheria za kimataifa katika kulinda mazingira.

Huu ni wakati wa msikamano wa kimataifa

Guterres amesema, "huu ni wakati wa kuamka na kukomesha ukiritimba huu , hisia zetu za kutoweza kufanya lolote zituelekeze kwenye unyenyekevu mkubwa, vitisho vya kimataifa vinahitaji umoja mpya na mshikamano.”

Katibu Mkuu amewapongeza wote walio katika msitari wa mbele kupambana na janga hili la COVID-19 kuanzia waugunzi na wakunga, hadi wafanyakazi wa maabara, wasimamizi na mamilioni ya wahudumu wa afya kote duniani ambao amesema wanaweka rehani Maisha yao ili kuokoa ya wengine.

Amewaambia washirika wa Baraza hilo kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kusimama na maelfu ya wafanyakazi wa shirika la afya duniani WHO ambao wanafanyakazi usiku na mchana kote duniani kuzisaidia nchi wanachama kuokoa maisha na kuwalinda walio hatarini, kutoa muongozo, mafunzo na vipimo muhimu, matibabu na vifaa vya kujikinga.

“WHO haina mbadala , inahitaji kuongezewa rasilimali ili liweze kutoa msaada hususan kwa nchi zinazoendelea ambazo zinapaswa kuwa hofu yetu kubwa. Tuna tungu kama udhaifu wa mifumo ya kiafya. Kuzisaidia nchi zinazoendelea sio suala la hisani au ukarimu bali ni suala la kuimarisha maslahi yetu. Mataifa ya Kaskazini  hayawezi kulishinda janga la COVID-19 hadi pale mataifa ya Kuisni yatakapolishinda kwa wakati mmoja.”

Ameikumbusha dunia kwamba huu si wakati wa kutupiana lawama na kunyoosheana vidole bali “ni wakati wa umoja kwa jumuiya ya kimataifa kufanyakazi pamoja kwa mshikamano kukomesha virusi hivi na athari zake”

Ameongeza kuwa dunia haiwezi kutafakari mustakbali ulioghubikwa na hofu na mashaka ni ama ilishinde janga hili kwa pamoja au ishindwe.

UN Photo/Eskinder Debebe
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akitoa taarifa kuhusu mlipuko wa COVID-19 mjini Geneva

Ushauri wa WHO umepuuzwa 
 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema nchi nyingi zimepuuza mapendekezo ya WHO “Na matokeo yake virusi vimesambaa duniani kote na sasa vinaelekea mataifa ya Kusini Kusini ambako athari zake zinaweza kuwa mbaya zaidi na tunahatarisha ongezeko la wimbi linguine la mlipuko.”

Ametoa wito kwa mataifa kushughulikia athari za janga hili la kiafya la COVID-19 , za kiuchumi na kijamii na kusema “endapo hatutokomesha kusambaa kwa virusi hivi basi uchumi hautotengamaa.”

Amesisitiza kwamba msaada unahitajika ambao utazifanya kaya ziendelee na maisha na biashara zisife. Amerejea wito wake kwa mataifa 20 tajiri ya G-20 kufikiria kuzindua fungu maalumu la kuchipuza tena uchumi la pato la kimataifa (GDP).

Ametoa wito pia wa msaada mkubwa kupitia shirika la fedha duniani IMF, Benki ya Dunia na taasisi zingine za kimataifa za fedha.

Walio hatarini wanahitaji msaada maalum

Katibu ameeleza kwamba wale walioathirika zaidi wanapaswa kupatia msaada wakiwemo wanawake, wazee, Watoto na wale wanaolipwa ujira mdogo miongoni mwa wengine.
Amesema wakati nchi zilizoendelea zinaweza kufanikisha haya zenyewe “ni lazima tuongeze rasilimali zilizopo ili kuzisaidia nchi zinazoendelea na wote tunalipa gharama kubwa ya janga hili.”

Akizungumzia wito uliotolewa na baadhi ya nchi wa kutaka uchunguzi wa jinsi gani tishio la viruzi hivi vipya vya corona vimesambaa kwa kasi , mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema ni mapema mno kufanya hivyo.

"Somo tutakalojifunza litakuwa muhimu sana katika kushughulikia changamoto nyingine kama hii ambazo zitajitokeza siku za usoni. Lakini sasa sio wakati muafaka. “
Amesisitiza kuwa huu ni wakati wa umoja kwa jumuita ya kimataifa, kufanyakazi Pamoja kwa mshikamano kukomesha virusi hivi na athari zake.
 

UNDP PAPP/Abed Zagout
Msikiti ukisafishwa Gaza ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID-19

Maisha ya watu 300,000 yamepotea na idadi inaongezeka

Naye mkurugenzi mkuu wa Who Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus akihutubia Baraza hilo amesema hadi kufikia leo WHO imearifu wagonjwa zaidi ya milioni 4.5 wa COVID-19 kote duniani na watu zaidi ya 300,000 wamepoteza maisha.
Ameongeza kuwa maambukizi hayo yamesambaa kwa kasi kama moto wa nyika na kuonya kwamba vipimo vya utafiti vya awali vya damu vinaonyesha kwamba kati yam to mmoja hadi wa wili miongoni mwa watu 10 inaonyesha wamekutana na virusi hivyo na kuchagiza kinga ya mwili kuchukua hatua ya kupambana navyo.

"Hata katika maeneo yaliyoathirika zaidi idadi ya watu wenye vijikinga maradhi sio zaidi ya asilimia 20 na katika maeneo mengi ni chini ya asilimia 10. Amesema Dkt. Tedros na kwa maneno mengine ni kwamba asilimia kubwa ya watu duniani bado wako kwenye hatari ya virusi hivi.”Amesisitiza kwamba hakuna nchi iliyosalimika na maambukizi ya virusi hivi, na wakati wengine ndio wakiwa katika kilele cha mlipuko huu, wengine ndio wanaanza kulegeza masharti ya hatua za kusalia nyumbani.

Maisha yaendelee kwa tahadhari kubwa

Dkt. Tedros amesema WHO inaelewa kikamilifu na kuunga mkono dhamira ya baadhi ya nchi kutaka kurejea katika Maisha ya kawaida na kurejea kazini lakini inawataka kufanya hivyo huku wakichukua tahadhari kubwa. “Na kwa kifupi ni kwamba tunataka dunia ijikwamue vyema haraka iwezekanavyo ndio maana tunazitaka nchi kuendelea kwa tahadhari kubwa. Nchi ambazo zinakwenda kwa kasi kubwa bila kuweka miundombinu ya kiafya ya umma kuweza kubaini na kudhibiti maambukizi zinajiweka katika hatari ya kutia dosari juhudi zake za kujikwamua na janga hili.”
Ameongeza kuwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linaendelea kuwasaidia wakimbizi wa Rohingya walioko Bangladesh dhidi ya janga hili la COVID-19.

© UNHCR
UNHCR inaendelea kuwasaidia wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh wakati huu wa janga la COVID-19

Afya ya kimataifa iko njiapanda

Kwa mujibu wa WHO janga hili linaloendelea la COVID-19 linahatarisha kurejesha nyuma hatua zilizopigwa kwa miongo kupambana na majanga mbalimbali ya kiafya ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, VVU, malaria, kifua kikuu, magonjwa yasiyo ya kuambukiza , matatizo ya akili, na polio miongoni mwa maradhi mengine.
Baraza hili la afya kikao cha 73, ambalo ni chombo cha maamuzi ya shirika la WHO safari hii linafanyika kwa njia ya mtandao na kwa siku tatu badala ya wiki mbili kama ilivyo desturi kwa sababu ya janga la COVID-19. Baraza hio la 73 la Afya Duniani lililoandaliwa na WHO mwaka huu linajikika na janga la COVID-19 na linashirikisha nchi zote wanachama 194. Litakunja jamvi Mei 21.

Wawakilishi kutoka nchi wanachama wa WHO wanatarajiwa kutoa taarifa zao zikilenga COVID-19 na masuala mengine ya kiafya yatajadiliwa wakati mwingine.

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud