Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana Somalia wajivunia kufunga mitambo ya sola

Amina Mahdi Abid, (wa pili kushoto) akijifunza jinsi ya kuunganisha na kufunga mitambo ya sola kwenye kituo kinachopatiwa msaada na UNICEF huko  Dollow, nchini Somalia.
© UNICEF/Mark Naftalin
Amina Mahdi Abid, (wa pili kushoto) akijifunza jinsi ya kuunganisha na kufunga mitambo ya sola kwenye kituo kinachopatiwa msaada na UNICEF huko Dollow, nchini Somalia.

Wasichana Somalia wajivunia kufunga mitambo ya sola

Wanawake

Nchini Somalia, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, linatekeleza mradi wa kuwezesha wasichana kupata stadi ambazo awali zilionekana kuwa ni za wanaume peke yao, hatua ambayo inalenga si tu kuongeza uwezo wa wasichana hao kupata kipato bali pia kutokomeza umaskini katika jamii zao. 

Mradi huo unatekelezwa kwenye mji wa Dollow uliopo jimbo la kusini la Gedo nchini Somalia ukilenga kuvunja mazoea ya kwamba kazi za kufunga mitambo ya sola zinafanywa na wanaume pekee.

Katika kituo hicho cha mafunzo, wanafunzi wa kike na wa kiume wanapatiwa stadi za ufundi mchundo ikiwemo ujenzi, uhandisi na ufundi bomba.

Miongoni mwa wanufaika ni Amina mwenye umri wa miaka 24 ambaye amekuwa akipata mafunzo ya miezi 5 ya kufunga mitambo ya umeme wa sola, awali alikuwa ana wasiwasi kwa kuwa watu walikuwa wakimuuliza ni kitu gani anajifunza katika karakana hiyo.

Amina anasema kuwa, “mara ya kwanza nilipofika hapa, watu walikuwa wananiuliza unaenda wapi? Mimi niliwajibu kuwa nataka kujifunza jinsi ya kuunganisha na kufunga mitambo ya umeme wa sola. Watu wataniuliza, wewe ni mwanamke, unaweza kuunganisha na kufunga mitambo ya sola? Basi, niliwajibu, ndio! Lakini nitajifunza na nitaweza kufunga mitambo ya sola.”

UNICEF inasema kuwa kuwapatia watoto wa kike na wasichana stadi za kufanya majukumu ambayo awali yalionekana si ya jinsia ya kike, kunawapatia ujasiri wa kuamini kuwa uwezo wao hauna ukomo.

Katika video ya UNICEF, Amina na wenzake wanaonekana kuunganisha sola kwenye bomba linalotoa maji na kwenye pipa bila kugusa jambo linalodhihirisha kuwa wana uwezo bila kujali jinsi yao.