Kwa kupiga namba 116 unaweza kuripoti unyanyasaji wa mtoto popote Tanzania 

12 Oktoba 2020

Mradi wa huduma ya simu namba 116 inayotumiwa bure kutoa taarifa taarifa za matukio ya unyanyasaji kwa mtoto, mradi unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA Tanzania unaendelea kuwa msaada wa kupambana na ukatili dhidi ya watoto nchini Tanzania.  

Michael Marwa ni Mkurugenzi wa huduma hiyo katika shirika la C-SEMA, wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike iliyoadhimishwa wilaya ya msalala, Segese, Shinyanga Tanzania, anaeleza namba hiyo inavyofanya kazi,“tunashirikiana kuendesha huduma ya simu kwa mtoto ambayo inatumia namba 116, namba hii inapatikana Tanzania nzima na hata Zanzibar na hii ni namba ambayo mtoto au mwanajamii anaweza akapiga simu kutoa taarifa inayohusu ukatili kwa mtoto au ukatili wa kijinsia kwamba kuna mtoto ambaye anafanyiwa unyanyasaji au ukatili wa kijinsia. ” 

Michael Marwa anasema takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa mkoa wa shinyanga ni moja ya maeneo yenye changamoto ya ndoa na mimba za utotoni ndio maana siku ya kimataifa ya mtoto wa kike nchini Tanzania imeadhimishwa katika halmashauri ya wilaya ya Msalala, Segese, mkoani Shinyanga, “changamoto kubwa ambayo inawahusu watoto wengi kwa ujumla ukiacha kuangalia wa kike na wa kiume ni ukatili wa utelekezwaji. Simu nyingi ambazo tunazipata kutoka ukanda huu ni simu ambazo watoto wametelekezwa kwa maana baba na mama wanaondoka au baba anaondoka bila kumpatia mtoto haki zake za msingi, haki ya elimu, haki ya afya, haki ya kwenda shule, haki ya malazi na vitu kama hivyo. Lakini maalumu sana au kesi zinazohusu watoto wa kike ni mimba za utotoni lakini pia zinafuatiwa na ndoa za utotoni na hii inasababisha watoto wengi kutokuendelea na shule hasa hasa shule ya sekondari ambapo tunajua kwamba shule ni mojawapo ya haki ya msingi ya maendeleo ya mtoto.” 

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter