Mkakati wa “Spotlight" unazaa matunda tuwekeze zaidi:UN

Mabinti wakifanya kampeni ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana huko El Salvador.
© UNICEF
Mabinti wakifanya kampeni ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana huko El Salvador.

Mkakati wa “Spotlight" unazaa matunda tuwekeze zaidi:UN

Wanawake

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto UNICEF, la mpango wa maendeleo UNDP  na linaloshughulikia masuala ya wanawake UN Women leo yamezindua ripoti ya matokeo ya mkakati wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana ujulikanao kama “sportlight Initiative” kwa mwaka 2020 na 2021. 

Wakizungumza na waandishi wa Habari mjini New York Marekani hii leo wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo wakuu wa mashirika hayo , Sima Sami Bahous mkurugenzi mtendani wa UN Women amesema “Hatua ya haraka ya Spotlight Initiative kurekebisha programu zake wakati wa janga la COVID-19 imesaidia kutoa huduma muhimu kwa wanawake na wasichana 650,000. Hatua hiyo imesisitiza na kuunga mkono utoaji wa huduma kamili wakati wa amri za watu kusalia majumani na kila kitu kufungwa.” 

Bahous ameongeza kuwa, "Hatua hizo ziliongeza juhudi za kuwaunganisha waathirika wa ukatili na watoa huduma muhimu licha ya vikwazo vya kutotembea na ilisaidia mashirika ya kiraia kukabiliana haraka na mabadiliko ya mazingira na kuimarisha huduma za mtandaoni, kama vile ushauri nasaha na huduma za simu." 

Mkuu huyo wa UN women pia amesema janga la COVID-19 bado linaendelea kuchochea ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika muktadha haki za wanawake kubinywa kote duniani. 

Amesisitiza kuwa “Sasa kuliko wakati mwingine wowote tunahitaji hatua Madhubuti ili kulinda mafanikio tuliyopata na kuhakikisha hayarudishwi nyuma, kwani sportlight initiative imedhihirisha nguvu ya kufanyakazi pamoja, kwa uratibu maalum ili kuhakikisha matunda yanapatikana katika shughuli zetu zinazohusiaha wadau mbalimbali. 

Wanawake waandamana kupinga unyanyasaji wa kijinsia nchini Ecuador.
UN Women/Johis Alarcón
Wanawake waandamana kupinga unyanyasaji wa kijinsia nchini Ecuador.

Haya ya kuendeleza uwekezaji  

Kwa upande wake Henrietta Fore, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video, asema kuwa mpango wa Spotlight unaonesha "haja endelevu ya uwekezaji ili kuzuia ukatili na kutoa matokeo yenye ufanisi." 

Fore ameongeza, kuwa "matokeo tunayozindua leo yanaonesha kile ambacho uwekezaji unaweza kufikia. Ukatili dhidi ya wasichana na wanawake unaweza kuzuilika na mabadiliko yanawezekana. Na lazima tuwaunge mkono wasichana na wanawake, wavulana na wanaume ambao wanaongoza mabadiliko haya." 

Mkuu wa UNDP Achim Steiner pia akizungumza kwa njia ya video katika uzinduzi huo amesema “Duniani kote, mpango wetu wa pamoja umechangia moja kwa moja katika uidhinishaji wa sheria na sera 84 ambazo zitachangia kupunguza unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana." 

Ameendelea kusema kwamba , “baadhi ya mikakati, mifumo ya kisheria, sote tunajua, haitoi hakikisho la kukomesha unyanyasaji  na ukatili wa kijinsia. Ni muhimu kukomesha hali hii inayouteketeza ulimwengu, bila kutaja moja ya kesi zake za kutisha na mauaji ya wanawake.” 

Steiner ameongeza, kuwa "kupitia uangalizi huo, tumeunga mkono, kwa mfano, nchi 17 katika Amerika ya Kusini, sio tu kufikia ushiriki kamili katika sheria dhidi ya mauaji ya wanawake katika kanuni za adhabu, lakini pia kuongeza kanuni ambazo zitawaadhibu wahalifu vikali zaidi." 

Na balozi wa ujumbe wa Muungano wa Ulaya kwenye Umoja wa Mataifa Olof Skook amesema "Ili kusonga mbele na kuendeleza mafanikio, tumeamua kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuendeleza  jukwaa la kimataifa la Spotlight, jukwaa ambalo litakuwa ni nguvu  ya pamoja ya kitovu cha maarifa, jumuiya ya utendaji, na chombo cha utetezi kilichoanzishwa kutokana na uzoefu wa vitendo. wa mpango wa Spotlight.”. 

Mpango huo unashukuru ukarimu wa Muungano wa Ulaya ambao ulitoa Euro milioni 500 ili kuanzishwa kwake.