Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la COVID-19 ni jinamizi kwa wazee-Guterres

Mwanaume Mzee anayefanya kazi ya kupiga viatu rangi ili kukimu mahitaji yake nchini Uturuki
© Eric Ganz
Mwanaume Mzee anayefanya kazi ya kupiga viatu rangi ili kukimu mahitaji yake nchini Uturuki

Janga la COVID-19 ni jinamizi kwa wazee-Guterres

Haki za binadamu

Janga la virusi vya corona au COVID-19 linasababisha hofu isiyoelezeka na madhila kwa wazee kote ulimwenguni.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo wakati wa uzinduzi wa sera kuhusu wazee kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

"Kiwango cha vifo kwa wazee kwa ujumla kiko juu na kwa wale wa umri wa Zaidi ya miaka 80 ni mara tano zaidiya wastani wa kote duniani.”

Zaidi ya athari za kiafya janga hilo linawaweka wazee katika hatari kubwa ya umasikini, ubaguzi na kutengwa.

Kuna uwezekano janga hili likawa na athari zaidi hasa kwa wazee katika nchi zinazoendelea.

Uzee maji ya moto

Akijitolea mfano Guterres amesema “Mimi mwenyewe nikiwa mzee, na mwenye majukumu ya kumuangalia mama ambaye ni mzee zaidi nitatiwa hofu kuhusu janga hili katika ngazi binafsi na kuhusu athari zake katika jamii na nchi zetu.”

Ameongeza kuwa leo hii tunazindua sera ambayo inatoa tathimini na mapendekezo ya kushughulikia changamoto. “Hatua zetu za kukabiliana na janga la COVID-19 lazima ziheshimu haki za binadamu na utu wa wazee.”

 Mambo manne ya kuzingatia

Katibu Mkuu amesema anatoa ujumbe katika masuala manne muhimu.
Mosi “ Hakuna mtu awe kijana au mzee ambaye ana utofauti. Wazee wana haki sawa ya kuishi na ya afya kwa alivyo kila mtu.” Hivyo uamuzi mgumu kuhudu huduma za afya za kuokoa maisha unapaswa kuheshimu haki za binadamu na utu kwa wote.

“Pili, wakati hatua ya kutochangamana ni muhimu , tusisahau kwamba sisi ni jamii moja na tunategemeana. Tunahitaji kuimarisha msaada wa kijamii na juhudi bora za kuwafikia wazee kupitia teknolojia ya kidijitali.”

Amesisitiza kwamba hili ni muhimu kwa wazee ambao huenda wakakabiliwa na madhila makubwa na kutengwa wakati huu wa hatua za kutochangamana na vikwazo vingine.

“Tatu, hatua zote za kijamii, kiuchumi na kibinadamu lazima zizingatia mahitaji ya wazee kikamilifu, kuanzia huduma za afya kwa wote hadi hifadhi ya jamii, ajira zenye hadhi na malipo ya uzeeni.”

Amesema asilimia kubwa ya wazee ni wanawake ambao wanauwezekano mkubwa wa kuingiza katika kipindi hiki wakiwa masikini na bila fursa za kupata huduma za afya. Hivyo sera ni lazima zilenge kukidhi mahitaji ya wanawake hao.

“Na nne hebu tuziwachukulie wazee kama watu wasioonekana au kutokuwa na uwezo wowote.”

Katibu Mkuu amesema wazee wengi wanategemea kipato na wanashiriki katika soko la ajira, maisha ya familia, katika kufundisha  na kusoma na kuangalia wengine hivyo sauti zao na uongozi wao ni muhimu.

Guterres ametoa wito kwamba “ili kutokomeza janga hili kwa Pamoja tunahitaji mshikamano wa kitaifa na kimataifa na mchango wa watu wote katika jamii wakiwemo wazee. Wakati tukijiandaa kujikwamua vyema katika janga hili tutahitaji hamasa na maoni ya kujenga jamii jumuishi, endelevu na za rika zote ambazo zinafaa kwa mustakabali wetu.”