Ukatili wa maneno na mtandaoni unakiuka haki za wazee lazima ukomeshwe:UN

15 Juni 2020

Ikiwa leo ni siku ya uelimishaji kuhusu ukatili dhidi ya wazee duniani Umoja wa Mataifa umesema ukatili wanaofanyiwa wazee kwa maneno au mtandaoni unakiuka haki za binadamu za watu wa kundi hilo na ni lazima ukomeshwe. 

Kauli hiyo imetolewa na mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa anayehusika na ufurahiaji wa haki zote za binadamu za wazee Claudia Mahler kupitia ujumbe wake wa siku hii akizitaka serikali zote na jumuiya ya kimataifa kuonyesha mshikamano wa kimataifa na kuweka bayana hatua za kuchukua ili kuzuia na kuwalinda wazee kutokana na ukatili wa kimwili na kisaikolojia ikiwemo kutelekezwa.

Ameongeza kuwa “wakati wazee wametajwa sana wakati huu wa janga la virusi vya corona au COVID-19, sauti zao, maoni yao na shuku na shaka zao bado hazijasikilizwa. Na wakati idadi ikiongzeka ya wazee wanaokifariki dunia majumbni, hospitali na katika vituo maalum vya kuwalea kote duniani , inaumiza na kusikitisha kuendelea kusoma lugha mbaya na ukatili unaowalenga wazee katika mitandao ya kijamii, na ukatili wa maneno unafanyika mara nyngi kwa kuwabagua wazee.”.

Mtaalam huyo amesisitiza kwamba ukatili wa maneno na mtandaoni una athari mbaya katika haki za binadamu za wazee na wakati mwingine kimwili na kiakili, pia unachagiza taswira mbaya au kusababisha hata machafuko na kutelekezwa kwa wazee.

Bi.Mahler amesema kauli za kuwaaibisha wazee kwenye vyombo vya Habari ni mashambulizi ya moja kwa moja kwa utu wa wazee.

Akitoa mfano wa hashtag iliyoambatana na janga la Corona ya “boomer remover” ikiwataka wazee kuweka rehami maisha yao ili kuokoa uchumi na vizazi vichanga ni wazi kwamba huo ni ubaguzi kwa wazee.

Kwa mantiki hiyo amesema “Sera ambazo zinaelemea mwenendo wa rika haziwezi kuvumiliwa na nazitaka nchi kufuatilia na kutekeleza hatua za kuepuka mitazamo ya kirika. Wazee wanahitaji kupata fursa ya mfumo wa uwajibikaji ambao utachukua hatua wakati haki zao za binadamu zinapokiukwa.”

Pia amezitaka jamii kupaza sauti wazee wanapotendewa ukatili  hususan wanawake na kutaka wajumuishwe katika majadiliano ya kupinga mifumo yote ya ukatili kwa watu hao.

Kwa mitandao ya kijamii ameitolea wito kutimiza wajibu wao na kutoruhusu ukatili kutendeka kwa kuandika ujumbe ambao unakiuka haki za binadamu za wazee.

Siku ya uelimishaji kuhusu ukatili wanaotendewa wazee hufanyika kila mwaka Juni 15.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter