Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kupambana na COVID-19 hazipaswi kufunika ukiukwaji wa haki za binadamu-Bachelet

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.

Hatua za kupambana na COVID-19 hazipaswi kufunika ukiukwaji wa haki za binadamu-Bachelet

Haki za binadamu

 Wakati serikali zinakabiliana na changamoto kubwa ya kuwalinda watu dhidi ya COVID-19, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amewataka wahakikishe haki za binadamu hazivunjwi kwa hatua za kipekee au za dharura.

Wakati serikali zinakabiliana na changamoto kubwa ya kuwalinda watu dhidi ya COVID-19, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amewataka wahakikishe haki za binadamu hazivunjwi kwa hatua za kipekee au za dharura.

Bachelet akizungumza hii leo mjini Geneva Uswisi, ameonya kuwa, “nguvu za dharura hazipaswi kuwa silaha ambayo serikali zinaweza kuitumia kudhibiti umoja, watu na pia kuendeleza muda wao madarakani. Inapaswa kutumika kukabiliana na ugonjwa huu hakuna zaidi.” 

Aidha Bi Bachelet ameongeza kusema kuwa mataifa yana uwezo wa kuzuia baadhi ya haki ili kulinda afya ya umma chini ya sheria ya haki za binadamu, na pia zina nguvu fulani za ziada ikiwa hali ya hatari ya kutishia maisha ya taifa itatangazwa. Katika hali zote mbili, vizuizi vinahitajika kuwa muhimu, sawia, na visivyo vya ubaguzi. Pia zinahitaji kuwa na muda wa ukomo na ziwekewe mipaka ya kutokupitiliza.

“Haki kadhaa ikiwemo haki ya kuishi, marufuku dhidi ya kuteswa na kutendewa vibaya, na haki ya kutokuwa kizuizini kinyjme cha sheria, zinatakiwa kuendelea kutumika katika hali zote.” Amesema Bachelet.

Ili kusaidia mataifa kushughulikia COVID-19, Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa jumatatu hii imetoa mwongozo mpya wa sera https://www.ohchr.org/Documents/Events/EmergencyMeasures_COVID19.pdf kuhusu dharura na hatua za kipekee.

Kamishina huyo wa haki za binadamu amesema kumekuwa na ripoti kadhaa kutoka katika maeneo tofautitofauti  kuwa polisi na vikosi vingine vya usalama vimekuwa vikitumia nguvu za ziada na wakati mwingine sumu kuwafanya watu wafuate utaratibu wa kubaki ndani au kutotoka nje. Ukiukwaji wa namna hiyo umefanyika mara kadhaa dhidi ya watu walioko katika kundi la watu masikini na walioko hatarini. 

“Kupiga risasi, kumtia nguvuni, au kumnyanyasa mtu kwa kuvunja sheria kwa sababu anatafuta chakula ni wazi kuwa haikubaliki na sio halali. Vivyo hivyo inafanya iwe ngumu au hatari kwa mwanamke kufika hospitalini kujifungua. Katika visa vingine, watu wanakufa kwa sababu ya utumizi usiofaa wa hatua ambazo zimedai kuwekwa ili kuwaokoa.” Amesema Bachelet.

Vilevile Bi Bachelet ameongeza kuwa katika baadhi ya nchi, maelfu wamewekwa kizuizini kwa kukiuka amri ya kukaa ndani, hatua ambayo si ya muhimu na isiyo salama. Jela na magereza ni mazingira ya hatari zaidi na mataifa yanatakiwa kujikita katika kumwachia yeyote ambaye kiusalama anaweza kuachiwa na pia wasishikilie watu wengine.

Pamoja na masuala mengine, kuhusu suala la kubana taarifa, Kamishina wa haki za binadamu amesema pamoja na umuhimu wa kupambana na taarifa za kupotosha lakini kufunga ubadilishanaji wa taarifa na mawazo sit u kwamba inakiuka haki za binadamu bali pia inadhoofisha imani. Taarifa za uongo kuhusu COVID-19 zinawaweka watu katika hatari kubwa, kama yalivyo maamuzi mabaya ya sera.