Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR DRC yahofia ikiwa mlipuko wa COVID-19 utatokea katika kambi za wakimbizi wa ndani

Walinda amani wa MONUSCO wameweka mikakati kudhibiti kuenea kwa COVID-19
MONUSCO/Michael Ali
Walinda amani wa MONUSCO wameweka mikakati kudhibiti kuenea kwa COVID-19

UNHCR DRC yahofia ikiwa mlipuko wa COVID-19 utatokea katika kambi za wakimbizi wa ndani

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR linasema vurugu na kukosekana kwa usalama vinavyoendelea nchini Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo, DRC vinaweza kusababisha ugumu kwa watu waliofurushwa kuweza kufikia vituo vya huduma ya afya kwa hivyo shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wake linafanya kila liwezekanalo kudhibiti maambukizi ya magonjwa kama vile COVID-19.

 

UNHCR inasema maeneo mengi na vituo ambavyo vinahifadhi watu waliofurushwa makwao vimefurika na hivyo kufanya suala la kukaakatika umbali kati ya mtu na mtu kuwa mgumu.

Hata hivyo shirika hilo linajitahidi kujaribu kutoa mafunzo kwa wakimbizi hawa wa ndani kuhusu namna ya kukaa mbalimbali kati ya mtu na mtu ili kujikinga na magonjwa. Katika kambi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC, katika eneo la Beni jimboni Kivu Kaskazini, Afisa mmoja anaonekana akiwaelekeza watu waliojipanga kwenye mistari, umbali unaofaa kati ya mtu na mtu. Afisa mwingine kutoka shirika la INTERSOS aliyeshika kipaza sauti anafundisha kuhusu virusi vya corona.

“Mnafahamu kuhusu huu ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona. Unaitwa COVID-19 

Watu wanaendelea kunawa mikono kwa maji tiririka kutoka katika ndoo zilizosambazwa na UNHCR na INTERSOS, wamevaa barakoa na wanapimwa joto la miili yao. Afisa anaendelea kuelimisha,

“Mnajua kuna magonjwa mawili. La kwanza ni lipi?”

Ebola.” Wananchi wanajibu kisha afisa anauliza tena, “na la pili?”, Wananchi wanajijibu, “corona”

“Kwa hivyo mnayafahamu.” Afisa anayeelimisha ameridhika kuwa elimu sasa imewafikia wananchi.

 

Vilevile pale inapowezekana, UNHCR, inaendeleza programu ambazo zimekuwa zikiendelea kama vile kuendelea na msaada wa fedha taslimu kwa wakimbizi wa ndani katika jimbo la Kivu Kaskazini ili waweze kupata mahitaji yao ya kila siku ikiwemo chakula, huduma ya afya na malazi. Shirika hilo linasema hivi sasa linatumia mfumo wa kutuma fedha kwa simu ili kupunguza kukutana na watu ana kwa ana. Tayari UNHCR imezipatia familia 5,900 simu za mkononi. Mama Kavugho Kahuko Solonita, ambaye ni mkimbizi wa ndani ya DRC anaeleza atakavyozitumia fedha hizo, “hizi zitanisaidia sana. Nitanunua blanketi. Nina mtoto wa kiume anayeitwa Kapule. Hazungumzi. Vitu vyetu vyote viliungua katika nyumba. Nitatumia fedha hizi pia kumnunulia nguo kwsababu hatuna chochote.”