Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asanteni wauguzi na wakunga na tuna deni kwenu – Guterres

Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Thomas Nybo
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Asanteni wauguzi na wakunga na tuna deni kwenu – Guterres

Afya

Leo ni siku ya afya duniani ambapo ujumbe ukiwa ni saidia wauguzi na wakunga.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema  maadhimisho ya mwaka huu hata hivyo yanafanyika wakati mgumu kwa kila mtu.
 Amesema anatambua mchango wa wahudumu wote wa afya ambao hufanya kazi kila uchao kulinda usalama kuanzia madaktari, wafamasia, mafundi hadi wasafishaji na madereva, akisema anatoa shukrani kwani wanajiweka hatarini wakati wa janga la sasa la virusi vya Corona au COVID-19.

Hata hivyo kwa kuzingatia mwaka huu ni wa wauguzi na wakunga, Bwana Guterres amesema kila mtu ana sababu  ya kushukuru kwa huduma na utaalam wa wauguzi na wakunga na kwamba yeye anatambua hivyo na zaidi ya yote, “wauguzi hubeba baadhi ya mizigo mkubwa kabisa ya huduma za afya. Wauguzi hufanya kazi ngumu na kwa saa nyingi, huku wakihatarisha kuumia, maambukizi na mzigo wa afya ya akili ambao unaambatana na kazi hiyo inayotia kiwewe. Mara nyingi hutoa faraja wakati wa mwisho wa maisha.”
 

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Wauguzi na wakunga asanteni sana!

Amesema wakunga hutoa faraja katika mwanzo wa maisha na kwamba wakati wa janga kazi yao inakuwa ngumu zaidi, wakati wakileta watoto wetu wachanga katika ulimwengu huu.

Ni kwa mantiki hiyo Katibu amesema, “Kwa wauguzi na wakunga wa dunia hii: Asanten kwa kazi yenu. Katika nyakati hizi za kiwewe, nasema kwa wahudumu wote wa afya: tuko pamoja nanyi na tunawategemea.”

Ametamatisha ujumbe wake akiwaeleza kuwa, “mnatufanya tujivunie, mnatuhamasisha. Tuna deni kwenu. Asante kwa mabadiliko mnayoyafanya, kila siku na kila mahali.”

Siku ya afya duniani huadhimishwa tarehe 7 mwezi Aprili kila mwaka na inatokana na azimio namba WHA/A.2/Res.35  la Baraza Kuu la shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO.