Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fikra za kikoloni katika kujaribu chanjo ya COVID-19 Afrika zikome- WHO

Kuna upungufu wa vifaa tiba katika maeneo mengi kote duniani.
UN Photo/Loey Felipe
Kuna upungufu wa vifaa tiba katika maeneo mengi kote duniani.

Fikra za kikoloni katika kujaribu chanjo ya COVID-19 Afrika zikome- WHO

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema ameshtushwa sana na kauli za wiki iliyopita kutoka kwa baadhi ya wanasayansi wakipendekeza kuwa majaribio ya kwanza ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 yatafanyikia Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi siku ya Jumatatu, Dkt, Tedros amesema,

(Sauti ya Dkt. Tedros)

“Kwa kweli nilishtushwa sana. Nikasema wakati huu ambapo tunataka mshikamano, kauli za kibaguzi kama hizo haziwezi kusaidia na ni kinyume na mshikamano. Afrika haiwezi na katu haitakuwa uwanja wa majaribio ya chanjo yoyote. Tutafuata kanuni zote kujaribu chanjo au dawa yoyote duniani kote,  kwa kutumia kanuni hiyo hiyo,  iwe ni Ulaya au Afrika au kwingineko, tutafuata kanuni hiyo na kama kuna umuhimu wa majaribio kwingineko kutibu binadamu, vivyo hivyo kwa usawa. Na  fikra za kikoloni sasa zikome na WHO katu haitoachia kitendo hicho kifanyike Afrika au kwingineko.”

Badala yake amesema taratibu sahihi za majaribio ya chanjo zitafuatwa na binadamu watatendewa kama binadamu kwa kuwa watu wote ni binadamu.

Ameongeza kuwa, ni jambo la kushangaza sana kauli kama hizo za kufanya majaribio ya chanjo ya COVID-19 Afrika zinatokana kwa wanasayansi katika karne hii ya 21 na wamelaani vikali.