UN yazindua ombi la dola bilioni 2 kusadia nchi maskini kukabili virusi vya Corona

Umoja wa Mataifa leo umezindua ombi la dola bilioni 2 ili kusaidia harakati za kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 katika nchi maskini zaidi duniani.
Uzinduzi huo umefanyika jijini New York, Marekani kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya video wakati huu ambapo idadi kubwa ya wafanyakazi wa ofisi ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini humo wanafanya kazi kutokea nyumbani ili kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.
Katika hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema nchi hizo maskini zaidi duniani ni zile ambako mifumo ya afya ni dhaifu na zinahifadhi watu waliofurushwa makwao kwa sababu ya mabomu, ghasia, mafuriko, wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa karatasi za plastiki au wamelundikana kwenye kambi za wakimbizi au makazi yasiyo rasmi.
“Watu hawa hawana nyumba au makazi ambamo kwamo wanaweza kujitenga na wengine ili kuepusha maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Guterres.
Ni kwa mantiki hiyo amesema fedha zinazoombwa zitaratibiwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura na majanga, OCHA, na fungu hilo linajumuisha maombi mapya pamoja na ya awali yaliyokwishatangazwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na wadau wake.
“Iwapo ombi hilo litachangiwa vizuri, litaokoa maisha ya wengi na kuwezesha mashirika ya misaada na yale yasiyo ya kiserikali kuwa na maabara bora ya kupima vifaa vya kutibu wagonjwa huku wakilinda wahudumu wa afya,” amesema Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa mpango huo pia unajumuisha hatua za ziada za kusaidia jamii ambazo zinaendelea kufungua milango ya nyumba na miji yao na kupokea wakimbizi akikumbusha kuwa, “tunahitaji kuchukua hatua sasa kuondoa madhara ya kibinadamu ya COVID-9. Tunahitaji kuendelea kusaidia maombi ya misaada ya kibinadamu ambayo watu milioni 100 wanategemea.”
Katibu Mkuu Guterres amesema kuwa, iwapo fedha hizo zitatumika ndivyo sivyo, basi itakuwa ni janga “kipindupindu kitasambaa, surua na homa ya uti wa mgongo. Viwango vya utapiamlo vitaongezeka, na hivyo kufutilia mbali uwezo wa mataifa hayo kukabiliana na virusi vya Corona.”
Ameongeza kuwa kuunga mkono ombi hilo ni muhimu kwa ajil iya kulinda afya duniani na ni jambo la kimaadili na ni kwa maslahi ya kila mkazi wa dunia.
Guterres ametoa wito kwa serikali kuliunga mkono akikumbusha kuwa wakati nchi tajiri nazo zinahaha kukabili virusi, nchi zilizo maskini ambako hata mifumo ya afya ni dhaifu, huduma za kujikinga na Corona kwa kunawa mikono na sabuni bado ni changamoto kubwa.
Mkutano huo kwa njia ya video umehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, Dkt. Tedros Ghebreyesus ambaye amesema kuwa “virusi hivi sasa vinaenea katika mataifa ambayo mifumo yao ya afya ni dhaifu na ambako tayari yanakabiliwa na majanga ya kibinadamu. Mataifa haya yanahitaji msaada wetu na pia kwa ajili ya kutulinda sote na kusaidia kuondokana na janga hili. Na wakati huo huo, tusipambana na janga hili huku tukisahau dharura nyingine za afya ya binadamu.”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoot, UNICEF, Henrietta H. Fore yeye akamulika watoto akisema kuwa, “watoto ni waathirika wasioonekana kwenye COVID-19. Vizuizi vya kutotembea, kufungwa kwa shule vinaathiri elimu yao, afya ya kiakili na kupata huduma muhimu za afya. Hatari za kukabiliwa na ukatili ni kubwa kuliko wakati wowote ule kwa wavulana na wasichana vile vile. Kwa watoto wakimbizi, au wanaoishi kwenye mizozo madhara yatakuwa makubwa kuliko tuliyowahi kushuhudia. Katu tusiwaangushe.”
Kwa upande wake Mratibu Mkuu wa misaada ya dharura ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa na Mkuu wa ofisi inayoratibu misaada, OCHA, Mark Lowcock yeye alianza kuchangia mkutano huo kwa kutangaza nyongeza ya dola milioni 60 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF.
“Mchango huo unafanya kiasi kilichotolewa na CERF kusaidia hatua za kibinadamu dhidi ya COVID-19 kufikia milioni 75. Mchango huu wa CERF, mkubwa zaidi kuwahi kutolewa na mfuko huo utaisaidia shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP kuhakikisha usambazaji wa bidhaa na usafirishaji wa wahudumu wa kibinadamu unaendelea” amesema Bwana Lowcock.
Halikadhalika fungu hilo la CERT litasaidia WHO kusaidia kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona na pia mashirika mengine ya kibinadamu kutoa msaada kwa waathirika zaidi kama vile wanawake na wasichana, wakimbizi, huduma za maji safi na salama na kujisafi, afya ya akili na mwili, lishe na ulinzi.