Skip to main content

Tuweke silaha chini na tupambane na adui mkubwa COVID-19:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres atoa wito kwa ajili ya kupambana na COVID-19
UN News/Daniel Dickinson
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres atoa wito kwa ajili ya kupambana na COVID-19

Tuweke silaha chini na tupambane na adui mkubwa COVID-19:Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ametoa wito wa kusitisha mapigano haraka kote duniani na nguvu zote kuzielekeza katika adui mkubwa wa sasa ambaye ni virusi vya Corona, COVID-19.

Katika wito wake maalum kupitia ujumbe wa video hii leo Guterres amesema “Dunia yetu inakabiliwa na adui wa pamoja ambaye ni COVID-19. Virusi hivi havijali kuhusu utaifa au ukabila , kikundi au imani. Vinatushambulia wote bila huruma.”

Wakati huohuo amesisitiza kwamba “vita vya silaha vimetawala duniani kote na wale wasiojiweza  kama wanawake na watoto, watu wenye ulemavu , waliotemgwa na waliotawanywa ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi.”

Ameongeza kuwa na watu hao ndio walio katika hatari kubwa ya kukabiliwa na athari mbaya kutokana na COVID-19.

Ameitaka dunia kutosahau kwamba nchi zilizoghubikwa na vita mifumo yake ya afya imesambaratika, wahudumu wa afya tayari ni wachache na mara nyingi wanalengwa na mashambulizi.

Amesema n abaya zaidi wakimbizi na watu wengine waliotawanywa na machafuko wako hatarini mara mbili.

Hivyo akasema “Hasira ya virusi inaonyesha upumbavu wa vita, ndio maana leo hii, ninatoa wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano haraka katika pembe zote za dunia. Ni wakati wa kuifunga migogoro ya silaha na kujikita pamoja kwenye mapambano ya kweli ya maisha yetu.”

Kisha akawageukia pande kinzani, akisema “Jiengueni kutoka kwenye uhasama, wekeni kando kutoaminiana na chuki, nyamazisheni silaha, komesheni mashambulizi ya makombora, malizeni mashambulizi ya anga. Hili ni muhimu sana katika kusaidia kutoa mwanya wa misaada ya kuokoa Maisha, kufungua njia kwa ajili ya diplomasia, na kuleta matumaini katika maeneo ya walio hatarini kwa COVID-19”.

Katibu Mkuu ametoa wito wa kuchukua msukumo wa umoja na mazungumzo ambayo taratibu amesema yanaanza kuchukua sura mpya miongoni mwa pande kinzani ili kuwezesha mtazamo wa pamoja wa kukabiliana na COVID-19. Hata hivyo amesema tunahitaji hatua zaidi ya hayo.

Tumalize madhila ya vita na kupambana na ugonjwa ambao unaisambaratisha dunia yetu. Hii inaanza kwa kusitisha mapigano kila mahali sasa. Hilo ndilo familia ya ubinadamu wetu inalihitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote.”